Marcelina Andrew Mkini mwenyekiti wa UWT wilaya ya Mufindi
Na Matukio Daima Media, Mufindi
Zikiwa zimepita siku tatu tangu mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan kukamilisha ziara yake ya kampeni mkoani Iringa, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Mufindi, Marcelina Andrew Mkini, amesema kuwa kazi kubwa na ya kihistoria iliyofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia inawapa matumaini makubwa kwamba kura za wagombea wengine hazitahesabika Mufindi, kwani wananchi wa wilaya hiyo wamejipanga kwa dhati kumpa kura za kutosha ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.
Mkini alisema kuwa UWT Mufindi inajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia, kwani serikali yake imeleta maendeleo makubwa yanayoonekana kwa macho ya kila mwananchi.
Alisema miradi mbalimbali ya maendeleo imeendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa, na kwa mara ya kwanza wananchi wa Mufindi wanahisi kuguswa moja kwa moja na keki ya Taifa kupitia uwekezaji na miradi ya kijamii inayotekelezwa wilayani humo.
Akizungumza kwa kujiamini, Mkini alisisitiza kuwa wanawake wa Mufindi sasa wako tayari kurejesha fadhila kwa Dkt. Samia kupitia sanduku la kura.
Alisema kwa miaka mingi wanawake walikabiliwa na changamoto kubwa hususan katika huduma za afya, lakini awamu hii imeondoa vikwazo hivyo.
“Wamepita marais wengi na kila mmoja alifanya kazi kubwa kwa wakati wake, lakini ni ukweli usiopingika kwamba Dkt. Samia ametenda makubwa ndani ya muda mfupi. Ameleta matumaini mapya kwa wanawake na jamii kwa ujumla.
Sasa hivi akina mama wajawazito hawapati tena tabu kama ilivyokuwa zamani, huduma za afya zimeboreshwa, zahanati na vituo vya afya vimekarabatiwa na kuongezewa vifaa.
Hii ndiyo sababu wanawake wa Mufindi wapo bega kwa bega naye kuelekea Oktoba 29,” alisema.
Mkini aliongeza kuwa maboresho hayo yamepunguza vifo vya mama na mtoto, jambo ambalo limekuwa kilio cha muda mrefu kwa jamii ya Mufindi. “Hii ni kazi kubwa ya kiukombozi kwa wanawake na familia kwa ujumla.
Hakuna tena mwananchi anayeweza kupuuza kazi ya Rais Samia kwa macho mawili,” alisema kwa msisitizo.
Mbali na sekta ya afya, Mkini alieleza kuwa wananchi wa Mufindi wameshuhudia hatua kubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
Alitolea mfano ujenzi wa barabara ya Nyololo–Kibao ambayo imekuwa kilio cha muda mrefu. Kwa sasa tayari kazi imeanza, na serikali imeahidi kuhakikisha barabara hiyo inakamilika ili kufungua zaidi fursa za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa eneo hilo.
“Kupitia mradi huu, wananchi wana matumaini mapya.
Wakulima sasa wataweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi, wafanyabiashara watanufaika, na huduma za kijamii zitapatikana kwa ufanisi zaidi.
Hakuna mwananchi atakayebaki nyuma katika safari hii ya maendeleo,” alisema Mkini.
Aidha, alizungumzia suala la madai ya wafanyakazi wa kiwanda cha Mgololo na Chuo cha MTC ambacho kwa muda mrefu kilikuwa kero kubwa kwa wastaafu na wafanyakazi waliostaafu.
Alisema serikali ya awamu ya sita imesikiliza kilio hicho na sasa imeahidi kuhakikisha madai yao yanashughulikiwa kwa haki.
“Kupitia hatua hii, wananchi wamejionea kuwa serikali ya Dkt. Samia ni sikivu na iko tayari kutatua changamoto zinazowakabili.
WanaMufindi wanaamini kabisa kuwa kero hii sasa iko kwenye mikono salama, na suluhisho la kudumu linakuja,” alisema.
Mkini alisema kuwa ahadi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo vimejenga imani kubwa kwa wananchi wa Mufindi, na hasa wanawake.
Alisisitiza kuwa hakuna shaka kwamba Oktoba 29 wanawake na wanaume watatoka kwa wingi kwenda kupiga kura, kuhakikisha kura zote za Mufindi zinamwendea Dkt. Samia.
“Wanawake wa Mufindi siyo tu wamejipanga wao pekee, bali wamepanga pia kuwaelimisha waume zao na vijana wao kushiriki kwa wingi.
Tumejipanga kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba, kijiji kwa kijiji, ili kila mwananchi aelewe umuhimu wa kuendelea kumpa nafasi Dkt. Samia aendelee kutekeleza dira yake ya maendeleo kwa Taifa,” alisema.
Mkini alisema kwa kuangalia kasi ya utekelezaji wa miradi ndani ya muda mfupi, wananchi wa Mufindi hawana wasiwasi wowote na ahadi zilizotolewa na Dkt. Samia.
Alisema miradi mingi imeanza kutekelezwa na matunda yake yanaonekana kwa macho ya kawaida, jambo linalowajengea imani kubwa wananchi.
“Rais wetu ni mtu wa vitendo, si wa maneno. Ahadi zake hazibaki kwenye karatasi, zinakuwa halisi kuuwa ndio maana wananchi kwa Mufindi hawana shaka, wanajua kinachosemwa kitafanyika hilo ndilo linalowafanya wasisubiri tena, bali kueendelee kuhamasisha kila mwananchi kumpa kura za kutosha,” aliongeza Mkini.
Mwenyekiti huyo wa UWT Mufindi alisema kuwa wananchi wa wilaya hiyo wameona matunda ya kazi kubwa iliyofanywa na Dkt. Samia ndani ya kipindi kifupi, na wanajua wazi kuwa kumpa nafasi nyingine ya kuongoza ni chaguo sahihi.
Alisema kuwa Oktoba 29 itakuwa siku ya kihistoria kwa wanawake na wananchi wote wa Mufindi, kwani kura zao zitakuwa majibu ya shukrani kwa kazi na upendo alioonyesha Rais Samia kwao.
“Kwa kweli kura za UWT Mufindi hazihesabiki, na Dkt. Samia hana sababu ya kuwa na shaka Tumeshikamana na tumedhamiria.. Wanawake wa UWT Mufindi ni silaha kubwa ya ushindi wake,”
0 Comments