Na Matukio Daima Media, Iringa
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kalenga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jackson Gidioni Kiswaga, amesema kuwa utendaji wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka minne unafanana kwa kiasi kikubwa na jitihada za kihistoria za shujaa wa Wahehe, Chief Mkwawa, kwa sababu zote zimejikita katika kuunganisha watu na kuwaletea maendeleo ya pamoja.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kalenga, Kiswaga alisema historia ya Chief Mkwawa ilijengwa katika dhamira ya kuunganisha Watanganyika na kuwatetea dhidi ya ukoloni, hali ambayo anasema inaendana moja kwa moja na jitihada za Rais Samia za kuunganisha Watanzania na kuwaletea maendeleo ya kitaifa.
“Kwanza nimshukuru sana Rais wetu kwa kufika Kalenga, lakini pia kwa kuniridhia kurudi tena kugombea Jimbo hili kupitia chama chetu. Hapa ulipofika ni eneo lenye historia kubwa, historia inayofanana na yako Wakati wa vita, Chief Mkwawa alikuwa na tabia ya kuungana na wenzake, na aliposhinda alirudi akamwaga mchanga aliochukua katika maeneo aliyopigania kwa lengo la kuunganisha Watanganyika. Ndio kazi ambayo pia wewe umeifanya kwa miaka minne kuunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja,” alisema Kiswaga.
Mafanikio yaliyopatikana Kalenga
Kiswaga alitumia nafasi hiyo kueleza baadhi ya mafanikio makubwa ambayo wananchi wa Jimbo la Kalenga wamenufaika nayo chini ya uongozi wa Rais Samia. Alisema moja ya sekta zilizoguswa kwa kiwango kikubwa ni miundombinu, ambapo miradi ya barabara imekuwa chachu ya kuunganisha jimbo na maeneo mengine ya mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.
“Kwa kipindi kifupi cha miaka minne, tumeshuhudia miradi mikubwa ya barabara ikitekelezwa. Mfano, barabara ya kwenda Ruaha National Park kupitia Kalenga, barabara ambayo hata Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuipanga, lakini haikuweza kufanyiwa kazi. Wewe uliposikia kilio chetu uliamua kutoa zaidi ya Shilingi bilioni 300 na ujenzi ukaanza mara moja,” alisema Kiswaga.
Aliongeza kuwa Rais Samia pia alifanikiwa kujenga barabara ya kiwango cha lami kutoka Iringa Mjini kuelekea Kilolo, mradi ulioigharimu zaidi ya Shilingi bilioni 60, huku sehemu kubwa ya barabara hiyo ikipita Jimbo la Kalenga. Vilevile, alitaja ujenzi wa barabara ya vijijini kutoka Wenda kwenda Mgama kwa gharama ya Shilingi bilioni 29 kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana.
Sekta ya elimu
Mbali na miundombinu, Kiswaga alisema sekta ya elimu pia imepata msukumo mkubwa katika jimbo hilo. Kupitia uongozi wa Dkt. Samia, kata mbalimbali zimepatiwa shule mpya, jambo lililopunguza changamoto za wanafunzi kutembea umbali mrefu.
“Katika Jimbo la Kalenga umetuletea shule nne mpya za sekondari, na sasa tuna jumla ya shule 24 katika kata 15. Ni jambo kubwa sana kwetu. Vilevile umetujengea madarasa 173 katika shule zetu, jambo ambalo limeongeza nafasi kwa wanafunzi wengi zaidi kuendelea na masomo yao kwa mazingira bora,” alisema Kiswaga.
Sekta ya kilimo
Akiendelea kueleza mafanikio, Kiswaga alisema jimbo hilo limekuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa ruzuku za kilimo zilizotolewa na Serikali. Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia, zaidi ya Shilingi bilioni 700 zilitolewa kama ruzuku, na sehemu ya fedha hizo iliwafikia wakulima wa Kalenga moja kwa moja.
“Jimbo letu lina wakulima wengi, na ruzuku hizi zimekuwa mkombozi kwao. Wamepata mbolea ya ruzuku kwa wingi na kwa wakati, jambo lililowasaidia kuzalisha chakula cha kutosha. Pia katika sekta ya umwagiliaji umetuletea Shilingi bilioni 13, mradi uliosainiwa mwezi Aprili, ambao utaongeza uzalishaji na kuhakikisha usalama wa chakula kwa wananchi wetu,” alisisitiza.
Sekta ya afya na nishati
Kiswaga pia aliipongeza Serikali ya Rais Samia kwa kuboresha huduma za afya katika Jimbo la Kalenga. Alieleza kuwa awali kulikuwa na vituo vitatu pekee vya afya, lakini sasa idadi hiyo imeongezeka kufikia vituo saba baada ya kujengwa vituo vipya vinne.
Katika sekta ya nishati, alisema maeneo mengi yaliyokuwa hayajafikiwa na umeme sasa yameunganishwa kupitia miradi ya REA, hali iliyobadilisha maisha ya wananchi vijijini na kuchochea shughuli za maendeleo.
Changamoto zilizopo
Hata hivyo, Kiswaga alitumia nafasi hiyo pia kuwasilisha changamoto na maombi ya wananchi wa Jimbo la Kalenga kwa Rais Samia. Alisema bado kuna vitongoji 15 ambavyo havijafikiwa na umeme, hivyo akaomba viongezwe katika miradi ijayo ya Energy Compact ili kuhakikisha wananchi wote wa jimbo hilo wananufaika.
“Tunaomba mradi wa umeme vijijini ukamilike katika vitongoji vilivyobaki ili wananchi wote wafikie huduma hii muhimu. Vilevile tunaomba uboreshwe mradi wa barabara ya kutoka hapa Kalenga kwenda Wasa, barabara ya kihistoria iliyotumika sana tangu enzi za ukoloni lakini hadi sasa haijakidhi viwango vya kisasa,” alisema Kiswaga.
Kiswaga alisema kuwa historia ya Kalenga ni kielelezo cha mshikamano wa Watanzania, na akasisitiza kuwa utendaji wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unaendana na urithi wa shujaa Chief Mkwawa katika jitihada za kuunganisha watu na kupigania maendeleo ya taifa.
“Wananchi wa Kalenga tumeshuhudia kwa macho yetu jinsi ulivyobadilisha jimbo letu. Umeleta miundombinu, elimu, kilimo, afya na nishati. Ni imani yangu kuwa utakapopewa tena ridhaa ya kuendelea kuongoza taifa hili, Kalenga na Watanzania wote kwa ujumla watanufaika zaidi. Kwa hakika uongozi wako ni mwendelezo wa jitihada za kihistoria za shujaa wetu Chief Mkwawa,” alisema Kiswaga.
0 Comments