NA WILLIUM PAUL, MWANGA.
MGOMBEA wa Ubunge wa Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro kupitia Chama cha Mapinduzi, Dkt. Ngwaru Maghembe amewaahidi wananchi endapo watamchagua atahakikisha wanapata mikopo yenye riba nafuu iweze kuwanufaisha mmoja mmoja na kuachana na mikopo kausha damu.
Dkt. Maghembe alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika katika kata ya Lembeni ambapo alisema kuwa, atakapochaguliwa atahakikisha anajikita katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja.
Mgombea huyo alisema kuwa, atahakikisha wananchi wanapata mikopo ambayo itawanufaisha wao wenyewe na sio taasisi za kifedha lengo likiwa ni kuleta maendeleo kwa wananchi wa Mwanga na Taifa kwa ujumla.
Kuhusu swala la kilimo, Mgombea huyo alisema kuwa atahakikisha wananchi wanapata miradi ya kisasa ya umwagiliaji huku pia akibainisha kuwa lipo tatizo la maji katika kata ya Lembeni na kuahidi kulipambania ili kupata ufumbuzi ambapo kwa sasa wananchi wanapata maji mara moja kwa wiki.
Akizungumzia swala la uchakavu wa shule katika kata hiyo alisema kuwa, kwa kushirikiana na Diwani wa kata w atahakikisha shule zinakarabatiwa kwani serikali imekuwa ikiendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule mpya pamoja na kuziboresha nyingine kwa kuongeza vidato vya tano na sita.
"Natambua vipo vitongoji bado havijafikiwa na umeme na kwa Mwanga vipo tisa hivyo nitahakikisha nashirikiana na Tanesco kupitia Rea kuhakikisha vitongoji vyote vinafikiwa na umeme" Alisema Dkt. Ngwaru.
Na kuongeza "ipo zahanati ya Lembeni bado haijamilika ili wakinamama wajawazito na wananchi kwa ujumla mpate huduma za afya karibu sasa mtakaponichagua kuwa Mbunge nitahakikisha hili nalibeba zahanati hii inakamilika".
Aidha Mgombea huyo aliahidi atakapochaguliwa atahakikisha anarudi kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi ikiwemo kuzibeba na kwenda kuzisemea Bungeni ili serikali iweze kuzitatua.
Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa kata hiyo, Arafat Mzee alisema kuwa, lipo eneo la ustawi wa jamii ambapo halina zahanati hali ambayo inawalazimu wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika kituo cha afya cha Lembeni na kuahidi kushirikiana na Mbunge kupata zahanati katika eneo hilo.
Mzee alisema kuwa, lipo tatizo la ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa katika kituo cha Afya cha Lembeni hivyo atahakikisha anaishauri serikali kwa kushirikiana na Mbunge kuhakikisha kituo hicho kinapata gari la kubebea wagonjwa.
Mwisho.
0 Comments