Header Ads Widget

DKT. MWINYI AVUKA MATARAJIO YA WADHAMINI AREJESHA FOMU ZEC


Dk. Mwinyi WAPINZANI WAGOMBEE UMAKAMO WA RAIS 

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo amerejesha fomu ya kuteuliwa kugombea nafasi hiyo katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Maisara.

Dk. Mwinyi, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, amekuwa mgombea wa kwanza kurejesha fomu hiyo baada ya kukamilisha masharti yaliyowekwa na ZEC, ikiwemo kuwapata wadhamini 200 katika kila mkoa.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kurejesha fomu, Dk. Mwinyi amesema Agosti 30 alikuwa wa kwanza kuchukua fomu na kufuatia utaratibu, alitembelea mikoa yote kupata wadhamini.

Ameshukuru Mwenyezi Mungu na kupongeza wanachama wa CCM waliojitokeza kwa wingi kumdhamini, ambapo idadi iliyohitajika ilivukwa zaidi kutokana na hamasa kubwa ya wanachama kutaka kuwa sehemu ya kumdhamini.

“Nawapongeza kwa dhati kwa utayari wao wa kufanya hivyo na hatimaye leo nimerudi kurejesha fomu yangu nikiwa wa kwanza. Namshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kukamilisha hatua hii muhimu katika uchaguzi wetu,” alisema.


Aidha, Dk. Mwinyi amebainisha  kuwa hatua kubwa ya kurejesha fomu imekamilika na sasa kinachosubiriwa ni uteuzi rasmi wa wagombea Septemba 11, kabla ya CCM kuanza kampeni zake Septemba 13.

Amenitumia  nafasi hiyo kuwaomba wagombea wenzake kuweka kipaumbele cha kuhubiri amani na kufanya kampeni za kistaarabu ili mshindi wa uchaguzi aweze kushika dola na kupeleka mbele maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Uchaguzi kutoka ZEC, Thabit Idarous Faina, amesema tume hiyo imetoa fomu kwa vyama 17 vya siasa ambapo hadi sasa mgombea mmoja pekee amerudisha.

Amefafanua  kuwa Septemba 10 saa 10 jioni ndio mwisho wa kurejesha fomu, huku uteuzi rasmi wa wagombea ukitarajiwa kufanyika Septemba 11 baada ya majina kubandikwa kwa saa 24.

“Tutabandika majina na ikiwa hakutatokea pingamizi yoyote, basi wote watashiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu,” alisema.

Aidha, ameongeza kuwa fomu zote zitakaguliwa na endapo kuna mapungufu, mgombea huita ili kufanya marekebisho.

 @Thabit Madai-Zanzibar


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI