Na Ashrack Miraji – Matukio Daima App
Same, 10 Septemba 2025 – Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, leo amewatakia heri wanafunzi wa darasa la saba wilayani humo walioanza rasmi Mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi, huku akielezea matumaini yake kuwa Wilaya ya Same itafanya vizuri kitaifa.
Akizungumza leo ofisini kwake mjini Same, Mhe. Mgeni aliwapongeza wanafunzi kwa hatua waliyofikia na kuwataka kujiamini na kusoma kwa umakini ili kufanikisha ndoto zao.
“Leo ni siku kubwa kwa watoto wetu. Ni siku ya kupima jitihada zao na za walimu wao. Nawapongeza kwa kufika hapa na nawatakia kila la heri. Tunaamini kuwa Same tutaibuka kidedea kwa kufanya vizuri kitaifa,” alisema Mhe. Mgeni.
Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza kuwa maandalizi yamefanyika vizuri, huku akiwataka wanafunzi kufuata maadili ya mitihani na kuepuka vitendo vyovyote vya udanganyifu. Alitoa wito kwa walimu na wasimamizi kuhakikisha mtihani unafanyika kwa utulivu na haki kwa wote.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wazazi, walezi, walimu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi chote cha maandalizi ya mitihani hiyo.
“Tunaishukuru jamii kwa kujitokeza kuwasaidia wanafunzi – iwe ni kwa chakula, usafiri, au kuwapatia mazingira tulivu ya kujisomea. Ushirikiano huu umeonyesha namna gani elimu ni ajenda ya pamoja,” aliongeza Mhe. Mgeni.
Mkuu huyo pia aliwahimiza wanafunzi kuendelea kuwa watulivu katika siku zinazofuata, kula vizuri na kupumzika vya kutosha ili waweze kuendelea na mitihani kwa ufanisi.
Mitihani hiyo ya Taifa kwa darasa la saba inatarajiwa kuendelea kwa siku mbili kuanzia leo, ikihusisha masomo mbalimbali ya msingi kama vile Kiswahili, Hisabati, Sayansi, Kiingereza na Maarifa ya Jamii.
0 Comments