Header Ads Widget

WANACCM 2,000 SONGWE WAJITOKEZA KUMDHAMINI RAIS SAMIA KUGOMBEA TENA URAIS.

 

Na Moses Ng'wat, Mbozi.

ZAIDI ya wanachama 2,000 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Songwe wamejitokeza kumdhamini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuwania tena nafasi ya urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.


Zoezi la udhamini limefanyika, Agosti 11, 2025, katika ofisi za CCM mkoani Songwe, mjini Vwawa, likiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe, Radwell Mwampashi, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, pamoja na viongozi wa kamati ya siasa ya Mkoa.


Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwampashi amesema idadi kubwa ya wanachama waliyojitokeza ni ishara ya mshikamano na imani waliyonayo kwa uongozi wa Rais Samia, hususan katika kusimamia miradi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.


Matukio Daima imeshuhudia makundi mbalimbali ya wanachama kutoka wilaya zote za Mkoa huo, wakiwemo vijana, wanawake na wazee, wakijitokeza kwa wingi kutoa udhamini.


Hata hivyo, Mwampashi alitumia fursa hiyo kufichua siri namna mkoa huo ulivyopataa   heshima ya kuwa miongoni mwa mikoa 10 nchini iliyopewa fursa ya kumdhamini mgombea huyo wa urais wa CCM, kutokana na kufanya vizuri katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambapo mkoa huo ulishika nafasi ya tatu kitaifa.


Awali, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Songwe, Yusuph Rajabu, alifafanua kuwa kati ya mikoa 32 ya kichama Tanzania Bara na Visiwani, Songwe imechaguliwa kutokana na rekodi yake nzuri ya kisiasa na kiutendaji.


"Tangu asubuhi tumeona makundi mbalimbali ya watu ambao ni wanachama, wafanyabiashara , Bodaboda na makundi ya jamii wakiwa wamekuja hapa kwa lengo la kundhamini mgombea wetu licha ya kwamba utaratibu ulihitaji wanachama 230 tuu" alifafanua Katibu wa Itikadi, Rajabu.


Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa, Michael Mbanga, alisema pamoja na muda mfupi wa maandalizi, muitikio wa wananchi ulikuwa mkubwa kutoka makundi mbalimbali yakiwemo waendesha bodaboda, wazee wa mila na vikundi vya kijamii.

Mkuu wa Mkoa Makame alisema mwitikio huo ni ishara ya kukubalika kwa Rais Dkt. Samia kwa makundi yote ya kijamii, kutokana na uongozi wake uliosheheni maridhiano ya kisiasa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.


"Baada ya Rais Dkt. Samia kuingia madarakani, ameendeleza miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, huku akirejesha utulivu wa kisiasa na kuimarisha mshikamano wa kitaifa," alisema Makame.


Wengi wa  wanaCCM waliozungumza na Matukio Daima wamesema wamejitokeza kwa wingi kwa kuwa wanataka kuona Rais Samia akiendeleza juhudi zake za maendeleo katika awamu ijayo.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI