Header Ads Widget

WADAU WAKUTANA KUJADILI UHIFADHI WA BONDE LA MTO KILOMBERO

Farida Mangube, Morogoro 

 Wadau wa uhifadhi na maendeleo katika Bonde la Mto Kilombero wamekutana  kujadili changamoto na fursa zilizopo katika kulinda ikolojia ya bonde hilo, huku wakitafuta mbinu za pamoja za kuhakikisha maendeleo na uhifadhi vinakwenda sambamba.

Mkutano huo umeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa ufadhili wa Shirika la African Wildlife Foundation (AWF) kwa kushirikiana na Muungano wa Uhifadhi wa Asili (IUCN).

Akizungumza nje ya kikao, Meneja wa AWF Clarence Msafiri amesema jukwaa hilo ni sehemu ya kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kuweka mikakati ya pamoja, kutatua changamoto bila migongano, na kuongeza ushirikiano. “Tunataka wadau wawe na sauti moja kuhusu changamoto na fursa zilizopo. Pia tunaleta pamoja watu wa uhifadhi na wale ambao shughuli zao zinaathiri au kugusa moja kwa moja masuala ya mazingira,” amesema.

Amebainisha kuwa Bonde la Mto Kilombero, pamoja na kuwa kitovu cha kilimo, lina utajiri mkubwa wa maliasili hata hivyo, ongezeko la watu limechangia misitu mingi kubadilishwa kuwa mashamba na makazi, jambo linalohitaji mipango bora ya matumizi ya ardhi ili kulinda mifumo ikolojia.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira, amesema kuwa mkutano huo umewezesha wadau kutambua shughuli zinazofanyika kwenye bonde, kujipangia malengo ya muda mfupi, wa kati na mrefu, na kutengeneza mikakati ya pamoja. “Tumejifunza kuwa hakuna namna ya kuhifadhi ikolojia bila mshikamano wa wadau wote. Tunatoa wito kwa mashirika na asasi kuendelea kuunga mkono juhudi hizi na kuzisambaza katika mabonde mengine nchini,” amesema.

Washiriki wa mkutano huo walikubaliana kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya mwaka jana, kuchambua changamoto zilizojitokeza, na kuweka hatua mahsusi za kusonga mbele, ikiwemo kutafuta ufadhili wa miradi inayolenga kulinda Bonde la Kilombero.

Mkutano huo umejumuisha wawakilishi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, halmashauri za wilaya za Kilombero na Ulanga na Kilosa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Bonde la Mto Kilombero ni miongoni mwa maeneo nyeti kiikolojia nchini Tanzania, likiwa makazi ya wanyamapori, kitovu cha kilimo, na chanzo muhimu cha maji kwa Mto Rufiji.




 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI