Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Kampuni ya DongFang Electric (DEC) imefanikiwa kuchepusha maji ya mto Malagarasi katika eneo la Igamba kijiji cha Mwamila wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ili kuanza ujenzi wa tuta la bwawa la kuzalisha umeme kutoka Mto Malagarasi.
Zoezi la kufunga rasmi njia ya awali ya mto huo na kuelekeza katika njia nyingine limeshuhudiwa na Mkurugenzi wa kanda ya Magharibi wa Shirika la uzalishaji na usambazaji umeme nchini (TANESCO), Richard Swai kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Razalo Twange.
Mkurugenzi wa kanda ya Magharibi wa Shirika la uzalishaji na usambazaji umeme nchini (TANESCO), Richard Swai akizungumza katika zoezi la kufunga mkondo wa asili wa mto Malagarasi ili kuweza kuchepushwa kuanza kwa ujenzi wa bwana la kuzalisha umeme katika eneo la Igamba wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma
Akieleza kutekelezwa kwa uchepushaji huo Kaimu Mhandisi Mkazi wa kampuni ya DEC, Han Wel alisema mpango huo wa kuchepusha mto ulipaswa ukamilike tarehe 27 Agosti mwaka huu lakini wamekamilisha jambo hilo siku 10 kabla ya muda wake ili kuwezesha kuanza ujenzi wa tuta la kukusanyia maji (Bwawa) ikiwa ni sehemu ya kuanza mradi wa ujenzi wa mradi huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Razaro Twange Mkurugenzi wa kanda ya Magharibi wa Shirika hilo, Richard Swai alisema kuwa uchepushaji huo wa mto ni hatua ya awali ya kupata sehemu kavu ili kujenga tuta la kupeleka maji kwenye mitambo ya kuzalisha umeme na kwamba hadi sasa mradi umefikia asilimia 10 na upo ndani ya wakati.
Swai alisema kuwa mradi huo utakapokamilika mwezi Oktoba mwaka 2027 utawezesha kuzalisha umeme wa mega watt 49.5 na kwamba kiasi hicho kitachangia kwa kiasi kikubwa gridi ya taifa sambamba na kuifanya kanda ya Magharibi kuwa mzalishaji na mchangiaji wa umeme kwenye gridi ya Taifa jambo ambalo kabla ya hapo halikuwepo.
Wakandarasi wa kampuni ya Dongfang Electric ya China wanaotekeleza mradi wa kuzalisha umeme kwenye bwana la Malagarasi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma
0 Comments