JESHI la Polisi nchini limewataka waandishi wa Habari Nchini kufanya kazi kwa umakini zaidi hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu kwa kuepuka Habari zenye kupandikiza chuki na kuvuruga Amani ya nchi.
Akizungumza leo wakati mdahalo wa ulinzi na usalama kwa waandishi wa Habari ulioandaliwa na Mtandao wa watetezi wa haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na umoja wa Klabu za waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime alisema ni wajibu kwa vyombo vya Habari kutimiza wajibu wao.
Alisema Jeshi la Polisi limejipanga kulinda waandishi wa Habari wakati huu wa uchaguzi pamoja na kuhakikisha amani ya wananchi wote wakati wa uchaguzi.
Alisema waandishi wanaofika kuripoti uchaguzi si vibaya kujitambulisha kwa wakuu wa Polisi wanaokuwepo kwenye mikutano ya kampeni ambao wamepewa jukumu la kuwalinda waandishi wanapotimiza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya kazi yao.
Alisema kuwa waandishi wanapaswa kutambua kuwa amani yetu ni wajibu wa kila mmoja kuilinda hivyo popote penye viashiria vya uvunjifu wa amani ni lazima kila mmoja kuwajibika kukemea na sio kuchochea.
0 Comments