Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema matumizi ya vipimo sahihi ni msingi muhimu wa maendeleo kwa mkulima, mfanyabiashara na Mtanzania kwa ujumla, akisisitiza kuwa Serikali haitaendelea kuvumilia vitendo vya udanganyifu kupitia mizani zisizo sahihi.
Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo (Nanenane) Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J.K. Nyerere mjini Morogoro, Chalamila alitoa pongezi kwa Wakala wa Vipimo (WMA) kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa katika shughuli za biashara nchini.
“Naipongeza sana Wakala wa Vipimo kwa kazi nzuri ya kuhakikisha vipimo sahihi vinatumika katika shughuli mbalimbali, hasa katika sekta ya kilimo na biashara. Wakulima na wafanyabiashara wanapaswa kuhakikisha wanatumia vipimo vilivyohakikiwa kwa mujibu wa sheria ili kulinda haki zao na za wateja wao,” alisema Chalamila.
Aliongeza kuwa matumizi ya vipimo sahihi si tu yanasaidia kuimarisha biashara bali pia yanachochea ustawi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Aliwataka wakulima na wafanyabiashara kuhakikisha wanawasiliana na Wakala wa Vipimo mara kwa mara ili kupata huduma ya uhakiki wa mizani na vipimo vyao.
“Serikali haitaki kuona wananchi wanadhulumiwa kutokana na mizani za kughushi. Tutawachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuchezea vipimo kwa manufaa binafsi. Haki ni msingi wa amani, na vipimo sahihi ni sehemu ya haki hiyo,” aliongeza.
0 Comments