Na Samwel Mwanga, Busega.
ZAIDI ya wananchi 5,000 wa vijiji vya Ngasamo, Ngunga, Mwamjulila, Mwamgoba na Malili wilayani Busega, Mkoani Simiyu, wapo mbioni kupata huduma ya maji safi na salama kupitia mradi wa ujenzi wa vioski vya maji wenye thamani ya Sh milioni 586.5.
Imeelezwa kuwa kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh milioni 584 zimetolewa na Serikali Kuu, huku wananchi wakichangia nguvu zao Sh milioni 2.5
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Busega, Mhandisi Daniel Gagala, amesema hayo leo Agosti 14, 2025 mbele ya kiongozi wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ussi, kuwa mradi ulioanza Mei 9, 2025, umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 30, 2025.
Amesema ujenzi wa Vioski vitano vinavyojengwa, kila kimoja kikiwa na koki tano na uwezo wa kuhifadhi lita 10,000 za maji, vitapunguza kwa kiasi kikubwa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata maji na kuongeza muda wa kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi na kwamba Mradi huo ni ukombozi kwa wananchi ambao hawatatembea tena umbali mrefu kufuata maji.
Amesema kuwa mradi huo unatekelezwa na mkandarasi ESTATE CONTRACTORS CO. LTD ya Dodoma na hadi sasa ameshalipwa kiasi cha Sh 355,216,763 kulingana na kazi alizofanya.
Esther John ni mkazi wa kijiji cha Ngasamo amesema kuwa walikuwa wakiamka alfajiri saa 11:00 kwenda kutafuta maji.
"Maji haya yatatuondolea mateso tuliyoyapata kwa miaka mingi. Tulikuwa tukiamka alfajiri kwenda kuteka maji mbali, sasa tutapata hapa hapa," amesema.
John Mayuma ni mfugaji katika kijiji cha Malili amesema kuwa kwa sasa hapati tena shida ya kutafuta maji kwa ajili ya mifugo yake.
"Mimi nafuga kuku na mbuzi. Sasa sitahangaika tena kuwatafutia maji mbali, nitajikita zaidi kwenye biasharua yangu," alisema John Manyama wa kijiji cha Ngasamo.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la Msingi kwenye ujenzi wa Mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ussi, ameipongeza utekelezaji wa mradi huo na kuwataka wananchi kuutunza kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Amesema kuwa miradi yote inayotekelezwa na RUWASA katika mkoa wa Simiyu ambayo imepitiwa na Mwenge wa Uhuru ni mizuri na imekidhi vigezo na ina lengo la kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama.
"RUWASA mkoa wa Simiyu niwape pongezi kutokana na kazi nzuri mnazozifanya tumepita katika miradi yenu yote iko vizuri na mnamsaidia Rais Samia Suluhu kutekeleza adhima yake ya kumtua mama ndoo kichwani,"amesema.
Mwisho.

0 Comments