MOROGORO:
HALMASHAURI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro imetangaza majina ya wagombea udiwani wa kata 203 walioshinda kura za maoni na wanapaswa kuendelea na mchakato huku kata 11 zikisubiri maamuzi ya vikao vya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu CCM Taifa kutokana na sababu mbalimbali.
Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Nuru Ngereja, ametaja kata hizo kuwa ni Mbuyuni, Mlimani, Lukobe, Mwembesongo, Kilakala, Mafiga na Mindu (Manispaa ya Morogoro); Ngerengere (Wilaya ya Morogoro Vijijini); Msolwa (Kilosa); Mtimbira (Malinyi) na Mlali (Mvomero).
Kwa mujibu wa Ngereja, wagombea wa kata hizo walishinda kura za maoni lakini wanakabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo za kimaadili na uwepo wa makundi ndani ya chama, hali inayolazimu chama kujiridhisha kabla ya kuwateua rasmi. Alisema vigezo vinavyotumika ni pamoja na kukubalika kwa mgombea kwa wananchi, umoja wa wanachama katika kata husika na kuepuka kigharimu chama iwapo mgombea mwenye tuhuma ataidhinishwa.
Ngereja ameongeza kuwa wagombea 203 walioteuliwa rasmi wanaweza kuendelea na mchakato wa kuchukua fomu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kupeperusha bendera ya CCM, huku akibainisha kuwa wagombea wa viti maalumu waliopitishwa kwenye kura za maoni wote wameteuliwa tayari.
0 Comments