Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Zaidi ya wafanyabiashara 100 mkoani Njombe wamefungiwa mashine zao za kielektroniki EFD kutokana na ujanja ujanja katika matumizi yake ikiwemo kuuza risiti badala ya kuzitumia kihalali hususani wafanyabiashara wa mazao ya misitu.
Katika Kikao kazi Cha watumishi wa TRA mkoa wa Njombe kikiwa na lengo la kuweka wazi mikakati mipya ya kuanza mwaka mpya wa fedha,Meneja wa Mamlaka hiyo Specioza Owure amesema kukamatwa kwa watu hao kumesaidia kuongeza mapambano katika udhiti wa ukwepaji kodi uliowasaidia kuvuka lengo.
Aidha Specioza amesema Kati ya Malengo ya kutakiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 35 wamefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 38 sawa na asilimia 107.51
Katibu tawala mkoa wa Njombe Judica Omary mbali na kupongeza jitihada hizo lakini ameonya kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa watumishi wa TRA.
Aidha Judica Ameiagiza TRA kwenda kufanya oparesheni kubwa ya kukagua wafanyabiashara wanaokwepa kutumia Mashine za kielektroniki kwani wanadidimiza taifa Katika kujiletea maendeleo.
Akoheki Mbapila ni Mchunguzi Mkuu Takukuru mkoa wa Njombe ambaye amesema wataanza kuwakamata maofisa wote wa TRA wanaoripotiwa na Wafanyabiashara kujihusisha na tuhuma za rushwa na kuwafikisha mahakamani.
Kwa upande wao wakazi wa Njombe wakiwemo viongozi wa Dini wamesisitiza mamlaka ya mapato kutoza kodi halali na sio kuwabambika na kuwafungulia kesi.
Kikao kazi hicho kinatajwa kwenda kuweka wazi mikakati ya kwenda kukusanya kodi katika mwaka mpya wa fedha ambao mkoa wa Njombe umepangiwa kukusanya shilingi bilioni 41.
0 Comments