![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dk. Adam Fimbo (picha ya Maktaba Mtandaoni) |
Na. Mwandishi Wetu. |
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imetoa taarifa kwa Umma juu ya kubaini uwepo katika soko wa Dettol za maji bandia zenye ujazo wa 50ml, 125ml, 250ml, 500ml na Lita 1 zinazotengenezwa kinyume cha Sheria (Njia haramu) na kubandikwa lebo kuonesha ni Dettol zilizo halisi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa Umma mapema leo Agosti 16, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dk. Adam Fimbo imebainisha kuwa:
'Napenda kuutangazia umma kwamba kupitia mifumo ya ukaguzi na ufuatiliaji wa bidhaa katika soko iliyowekwa imebaini uwepo katika soko wa Dettol za maji bandia zenye ujazo huo tajwa.
Utengenezaji wa Dettol hizo bandia umebainika kufuatia taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa na TMDA na kisha ukaguzi uliofanywa kwa pamoja na Jeshi la Polisi katika nyumba moja ya kulala wageni inayoitwa New Kishimbe Lodge iliyopo Mtaa wa Namanga, Kahama mjini, mkoa wa Shinyanga." Imeeleza taarifa hiyo na kuongeza:
"Katika nyumba hiyo kulikutwa malighafi mbalimbali zikiwemo vifaa, kemikali na vyombo kama vile chupa tupu za Dettol, lebo, rangi, madumu makubwa na vimiminika (liquid foams) katika chumba kimojawapo walichokuwa wanaishi raia wawili (2) kutoka nchi jirani ambao wanatuhumiwa kushiriki katika uhalifu huo." Imebainisha taarifa.
Aidha, TMDA imetoa maelezo ya namna ya kutambua Dettol bandia.
![]() |
Maelezo ya jedwari katika taarifa ya TMDA kwa Umma. |
"Kutoka kubainika kwa Dettol hizi bandia, TMDA inapenda kuwashauri wananchi wote wanaotumia Dettol za maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kuuwa vijidudu kuangalia kwa makini lebo zake na endapo watatilia mashaka watoe taarifa kwenye Ofisi za TMDA zilizo karibu au Kituo cha Polisi.
Aidha, wafanyabiashara wanaojihusisha na ununuzi wa bidhaa hizi, wanaelekezwa kununua Dettol kutoka katika vyanzo halisi na kupewa risiti kwa manunuzi waliyofanya.
Hata hivyo, Watuhumiwa waliohusika na uhalifu huu wamefikishwa katika vyombo vya usalama na tararibu za kuwafikisha Mahakamani zinaendelea ili kuweza kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
Pia TMDA inatoa onyo kwa kampuni, kikundi, mitandao au mtu yeyote anayejihusisha na utengenezaji, usambazaji au uuzaji wa dawa ikiwemo vipukusi (antiseptics and disinfectants), vifaa tiba na vitendanishi duni na bandia kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha, TMDA inaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa TMDA au Vituo vya Polisi wanapobaini uwepo wa ukiukwaji ya Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219 ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa lengo la kulinda afya ya jamii.
0 Comments