Na. Mwandishi Wetu, Mufindi.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti Sao Hill umeendesha semina maalum kwa wavunaji wa miti na wadau wa sekta ya misitu, kwa lengo la kuwapa elimu kuhusu sheria, kanuni na taratibu za uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu.
Semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shamba hilo, ililenga kuwakumbusha wadau hao kuhusu umuhimu wa kufuata miongozo rasmi ya kisheria kabla, wakati na baada ya shughuli za uvunaji wa miti, ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, alisema kuwa ni muhimu kwa TFS na wadau wa misitu kukutana mara kwa mara ili kujadili namna bora ya kutekeleza shughuli za uvunaji kwa kuzingatia sheria zilizopo.
“Uvunaji na usafirishaji wa rasilimali za misitu katika mashamba ya serikali unaongozwa na sheria, hivyo ni muhimu tuendelee kukaa pamoja kujadili utekelezaji wake kwa ufanisi,” alisema Mhifadhi Yoramu.
Alisisitiza umuhimu wa waendesha shughuli hizo kuwa na nyaraka halali katika maeneo ya kazi, ili kuepuka usumbufu wakati wa ukaguzi, sambamba na kuchukua tahadhari dhidi ya matukio ya moto yanayoweza kusababisha madhara kwa mazingira na rasilimali.
Aidha, alieleza kuwa TFS itaendelea kuboresha huduma kwa wadau wake, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya barabara, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuboresha muda wa utoaji huduma kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa TFS Wilaya ya Mufindi, CO I Maria Karawa, alisisitiza umuhimu wa kutumia nyaraka sahihi zinazolingana na mifumo rasmi ya utoaji wa vibali na leseni kwa ajili ya kusafirisha mazao ya misitu kutoka eneo moja kwenda jingine.
Aliongeza kuwa ni wakati sasa kwa wadau hao kuwekeza katika teknolojia za kisasa kwa ajili ya uchakataji wa mazao ya misitu ili kuongeza tija na faida katika uzalishaji.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wavunaji wa Shamba la Miti Sao Hill, Bw. Obadia Kalenga, aliishukuru TFS kwa kuendelea kuratibu vikao hivyo, akisema kuwa vimekuwa msaada mkubwa kwa wadau wapya na wa muda mrefu kuelewa sheria na miongozo ya biashara ya mazao ya misitu.
“Semina hizi ni muhimu kwa wadau wote, wapya na waliopo kwa muda mrefu. Tunaiomba TFS iendelee na utaratibu huu mara kwa mara ili kuhakikisha sheria zinaeleweka vizuri,” alisema Bw. Kalenga.
Semina hiyo ilihusisha wahifadhi kutoka TFS – Shamba la Miti Sao Hill, ofisi ya Wilaya ya Mufindi, Umoja wa Wavunaji wa Miti Sao Hill, pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya misitu kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mufindi.
0 Comments