Mwandishi Wetu, Mufindi
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kwa kushirikiana na taasisi kutoka ndani na nje ya nchi, wameanza mchakato wa kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora za miti ili kukuza misitu ya viwanda na kuhifadhi mazingira.
Hayo yamejiri jana Agosti 6, 2025 katika Shamba la Miti Sao Hill, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, wakati wa ziara ya pamoja kati ya Kurugenzi ya Mbegu ya TFS na washirika wake wa kimataifa wakiwemo FORLAND Tanzania, TAPIO kutoka Finland na Chama cha Wahitimu wa Sayansi ya Misitu Tanzania (TTGAU).
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhifadhi Mkuu wa TFS, Dkt. Fortunate Senya, alisema lengo kuu ni kuhakikisha mbegu bora za miti kama mikaratusi na misindano zinazalishwa kwa viwango vya kitaifa na kimataifa, kwa ajili ya kuhudumia mashamba ya miti ya viwanda na kuleta tija kiuchumi na kimazingira.
“Tumejionea namna miche ya miti iliyoboreshwa inavyokuza kwa ufanisi katika bustani ya miche ya Irundi. Hii ni hatua muhimu kuelekea uhakika wa mbegu bora, hasa kwa mashamba yanayohitaji kurejeshwa baada ya kuvunwa,” alisema Dkt. Senya.
Katika ziara hiyo, timu ilitembelea pia Tarafa ya Pili ya Shamba Ihefu, ambapo walikagua shamba maalum la kuzalisha mbegu za mikaratusi.
Wataalamu walibainisha mafanikio pamoja na changamoto zinazojitokeza, huku wakisisitiza haja ya kuweka mikakati madhubuti kabla ya kuanzishwa kwa mashamba mengine mapya ya uzalishaji wa mbegu.
Aidha, wadau hao walionesha kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na TFS katika kulinda mashamba dhidi ya majanga ya moto hasa wakati wa kiangazi, jambo walilolieleza kuwa ni sehemu muhimu ya usimamizi endelevu wa misitu.
Kwa mujibu wa TFS, Shamba la Miti Sao Hill ni miongoni mwa mashamba yanayonufaika na mbegu bora zinazozalishwa na vituo vya taasisi hiyo kupitia ushirikiano wa kimkakati na wadau wa uhifadhi. Mbegu hizo hutumika pia kupunguza utegemezi wa misitu ya asili na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wao, wawakilishi wa TAPIO Finland na FORLAND wamesema Tanzania ina fursa kubwa ya kuwa kinara katika uzalishaji wa mbegu bora barani Afrika, endapo utawekwa mkazo katika utafiti, teknolojia na usimamizi shirikishi.
0 Comments