Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki kikao cha awali cha maafisa waandamizi cha Jukwaa la Majadiliano kati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Serikali ya Marekani kilichofanyika Antananarivo, Madagascar Agosti 13, 2025.
Akitoa neno la ufunguzi wa majadiliano hayo, Naibu Katibu Mtendaji wa SADC anayeshughulikia ushirikiano wa Kikanda, Bi. Angeles N'Tumba alisema kikao hicho ambacho ni cha kwanza kufanyika, kitajadili miongozo ambayo SADC na Marekani wataitumia katika ushirikiano wao ambao umelenga maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na amani na usalama, afya, uchumi na usimamizi wa rasilimali kama vile nishati na madini.
Mwakilishi wa Serikali ya Marekani ambaye ni Naibu Katibu Mkuu anayeshugulikia masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Melanie H. Higgins ameihakikishia SADC kuwa licha ya mabadiliko ya Sera katika Serikali ya Marekani, nchi hiyo imedhamiria kwa dhati kushirikiana na SADC na ndiyo maana yeye na ujumbe wake wametumwa kushiriki kikao hicho.
Ameongoza kuwa Marekani ipo tayari kushirikiana na SADC kutatua changamoto zinazoikabili kanda hiyo hususan zile zinazorejesha nyuma utekelezaji wa miradi ya maendeleo na amani na usalama.
Inaelezwa kuwa jukwaa hilo la majadiliano ni kielelezo cha dhamira ya dhati na ya pamoja kati ya SADC na Marekani katika kukuza na kuimarisha ushirikiano endelevu, mtangamano wa kikanda na kuibua fursa za kiuchumi kwa manufaa ya pande zote.
0 Comments