Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo, imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wanufaika 762,291 nchi nzima, kwa kuwasaidia kupata mikopo kupitia taasisi za kifedha bila hitaji la dhamana kubwa.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dodoma kwenye maonesho ya wakulima na wafugaji Kitaifa Rosemary Gordon Afisa Biashara wa TADB anayesimamia mfuko huo, alieleza kuwa mfuko huo unatekelezwa kwa ushirikiano na benki 13 za biashara, benki za ushirika, na taasisi nyingine za kifedha nchini.
“Mfuko huu unahakikisha kuwa wakulima wadogo, hata wale wasio na dhamana ya kutosha, wanapata mikopo ya kuwawezesha kuendesha shughuli zao za kilimo kutoka shambani hadi sokoni,” alisema Gordon.
Alisema mikopo inayodhaminiwa na mfuko huo husaidia wakulima kununua pembejeo kama mbegu, viuatilifu na mbolea, pamoja na dhana za kilimo kama matrekta na pampu za umwagiliaji (pawatila).
Pia amesema mfuko unahusisha wakulima wanaojihusisha na uchakataji wa mazao, wauzaji na wanunuzi wa mazao.
Aidha, Gordon alibainisha kuwa mfuko huo unawahudumia wakulima, wafugaji na wavuvi kote Tanzania Bara na Visiwani, na hadi sasa umeshatoa dhamana ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 5.5 kwa dhana za kilimo, na shilingi bilioni 197 kwa upande wa pembejeo.
“Tunahamasisha wakulima, hasa wanawake na vijana, kuchangamkia fursa hii kwani kwa kawaida, tunatoa dhamana hadi asilimia 50, lakini kwa miradi ya vijana na wanawake yenye kuzingatia mabadiliko ya tabianchi, dhamana hufikia hadi asilimia 70,” alifafanua.
Kwa upande wake, Mariam Leonard, Afisa Biashara wa TADB Kanda ya Kati, alisema benki hiyo imeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.1 kwa wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, ikiwa ni pamoja na wazalishaji, wachakataji na wasambazaji wa mazao.
Alitoa pongezi kwa wakulima kwa kuendelea kurejesha mikopo kwa wakati, hali inayochochewa na elimu wanayopewa kabla ya kupata mikopo.
“Muitikio wa urejeshaji uko vizuri. Wadau wengi wanazingatia masharti ya mikopo kwa sababu tunawapa elimu kabla ya kuwakopesha, jambo ambalo limeongeza uaminifu katika sekta hii,” alisema Mariam.
Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo ni mojawapo ya mikakati ya TADB ya kuondoa changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogo na kuimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.
Mwisho
0 Comments