Header Ads Widget

MATONYA: KILIMO, UFUGAJI NA USHIRIKI KUINUA WANANCHI MUFINDI KUSINI

MATONYA: KILIMO, UFUGAJI NA USHIRIKI KUINUA WANANCHI MUFINDI KUSINI


Na Matukio Daima Media, Mufindi

Mgombea wa nafasi ya ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Mufindi Kusini, Chavala Yohannes Matonya, ameendelea kujipambanua kama kiongozi mwenye maono ya kuleta mapinduzi ya kweli kwa wananchi wa jimbo hilo kupitia sekta ya kilimo, ufugaji, ushirika na miundombinu.

Akizungumza katika mikutano mbalimbali ya kampeni ya kuomba kura za maoni ndani ya CCM, Matonya amewaomba wanachama wa chama hicho kumpa ridhaa ya kuwa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CCM ili aweze kutimiza ndoto yake ya kulitoa jimbo hilo kutoka katika hali ya utegemezi wa uchumi wa kizamani na kulipeleka kwenye maendeleo ya kisasa yanayozingatia ushirikishwaji wa wananchi katika uzalishaji.


"Mufindi Kusini ni hazina kubwa ya uchumi wa kilimo, misitu, mifugo na watu wenye nguvu ya kazi, lakini tumekuwa tukikwama kwa sababu hatujawahi kupata kiongozi atakayesimamia rasilimali hizi kwa manufaa ya wananchi. Mimi, Chavala Yohannes Matonya, nimejipanga kubadilisha hali hiyo," alisema Matonya mbele ya maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza.

Alisema kuwa ajenda yake kuu ni kuhakikisha wananchi wa Mufindi Kusini wanawezeshwa kiuchumi kupitia vikundi vya ushirika vya kilimo, ufugaji na biashara ya mazao ya misitu, huku akihakikisha serikali inaleta maendeleo ya kweli kupitia barabara, maji, elimu, afya na teknolojia vijijini.

BARABARA YA MAFINGA-MTWANGO HADI MGOLOLO: DAMU YA UCHUMI

Katika kueleza vipaumbele vyake vya kipaumbele, Matonya alisisitiza kuwa barabara ya Mafinga - Mtwango hadi Mgololo, pamoja na ile ya Nyigo - Nyololo hadi Kibao Ziroziro ni uti wa mgongo wa maendeleo ya wananchi wa Mufindi Kusini, lakini zimekuwa ni kilio cha muda mrefu kutokana na kutopewa kipaumbele na viongozi waliopita.

"Barabara hii ni kila kitu kwa wananchi wa Mufindi Kusini. Kupitia barabara hii, wakulima wanapeleka chai, maharage, matunda, mbao na mazao mengine sokoni. Hata wagonjwa na wanafunzi hutumia barabara hiyo. Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa kwa miaka mingi ahadi zimekuwa zikitolewa lakini utekelezaji wake umekuwa ni ndoto ya mchana," alisema Matonya kwa masikitiko.

Aliongeza kuwa kila mbunge aliyepita amekuwa akitoa ahadi kuhusu ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, lakini hakuna hatua yoyote ya msingi iliyochukuliwa. Matonya amesema kuwa endapo atapewa nafasi ya kuwa mbunge, atahakikisha barabara hiyo inaingia katika mipango ya utekelezaji wa serikali kwa sababu ndiyo nguzo ya uchumi wa wananchi wa Mufindi Kusini.

"Nataka kuwaambia wananchi wenzangu wa Mufindi Kusini – kama mnataka kilio hiki cha muda mrefu kifike mwisho, basi ni wakati sasa wa kuchagua kiongozi ambaye hawezi kuchoka kuisemea barabara hii ndani ya Bunge na nje ya Bunge. Nitahakikisha barabara hii inaingizwa kwenye mpango wa maendeleo wa taifa na ujenzi wake unafanyika haraka," alisisitiza.

KILIMO BIASHARA NA UFUGAJI WA KISASA

Mbali na suala la barabara, Matonya amesema kuwa atahakikisha anasimamia kwa vitendo mageuzi katika sekta ya kilimo na ufugaji kwa kuwahamasisha wananchi kujiunga na vikundi vya ushirika na kuwajengea uwezo wa kufanya kilimo cha kisasa chenye tija na faida.

Amesema kuwa Mufindi Kusini ina mazingira bora ya kilimo cha chai, maharage, mahindi, viazi, parachichi, pamoja na matunda mbalimbali yanayoweza kusafirishwa hata nje ya nchi, lakini bado wakulima wanakosa elimu, pembejeo na masoko ya uhakika.

Katika sekta ya ufugaji, Matonya amesema kuwa atawasaidia wananchi hasa vijana na wanawake kuingia katika ufugaji wa kibiashara wa kuku, mbuzi, na ng’ombe wa maziwa, huku wakisaidiwa na halmashauri kupata chanjo, mbegu bora na mitaji.

"Tutaleta wataalamu wa ugani hadi vijijini, tutaweka mfumo wa upatikanaji wa pembejeo na mbegu bora kwa wakati, tutaanzisha ushirika wa wakulima wa kijiji hadi kijiji na kuhakikisha mazao yanapata soko la uhakika. Tukiwekeza vizuri katika kilimo na ufugaji, ajira kwa vijana itazaliwa moja kwa moja," alisema Matonya.

USHIRIKA NA KUWEZESHA WANANCHI KIUCHUMI

Akizungumza kuhusu dhana ya ushirika, Matonya alisisitiza kuwa bila kuimarisha ushirika, wananchi wa Mufindi Kusini wataendelea kunyonya na walanguzi wa mazao. Amesema kuwa kupitia ushirika wa kweli, wananchi wataweza kuuza bidhaa zao kwa bei ya ushindani na kupata faida halisi.

"Tutaunda vyama vya msingi vya ushirika kwa wakulima wa chai, maharage, parachichi, pamoja na wafugaji. Ushirika huu utakuwa chombo cha kupata mikopo, mafunzo, masoko na ushauri wa kitaalamu. Hatutarajii tena wakulima wetu kuuza mazao yao kwa hasara," alifafanua.

Matonya amesema pia atahakikisha vijana wa jimbo hilo wanashirikishwa kikamilifu katika uchumi wa kijani kwa kuwawezesha kupitia mikopo ya halmashauri, mafunzo ya stadi za kazi na kujiajiri kwenye kilimo biashara na miradi ya ufugaji wa kisasa.

MWITO KWA WANANCHI

Matonya aliwataka wanachama wa CCM kumpigia kura za kutosha ili aweze kupita katika mchakato wa kura za maoni na hatimaye kuwa mwakilishi wao bungeni. Alisema anatambua kuwa kazi ya ubunge ni ya uaminifu, uwajibikaji na usimamizi wa haki za wananchi.

"Nataka niwe sauti ya wananchi wa Mufindi Kusini ndani ya Bunge nipo tayari kupigania haki zenu kwa kila hali. Sitachoka, sitarudi nyuma hadi pale mtakapoona barabara zenu zimejengwa, mazao yenu yamepata soko na kipato chenu kimeongezeka. Naombeni kura zenu kwa ajili ya mustakabali wa vizazi vyetu," alihitimisha kwa matumaini.

Wananchi wengi waliohudhuria mikutano yake wameonesha kuguswa na maono yake, wakisema kuwa Matonya ameonesha tofauti kubwa na wagombea wengine kutokana na umakini wake, mpangilio wa hoja na uelewa wa changamoto zinazowakabili.

Jimbo la Mufindi Kusini limeendelea kuwa sehemu muhimu ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na misitu nchini, hivyo kupata kiongozi mwenye maono na uwezo wa kusimamia rasilimali hizo ni jambo linalosubiriwa kwa hamu na wananchi.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI