Header Ads Widget

MAREKANI YASHTAKI RAIA WA TANZANIA NA KENYA KWA NJAMA YA KUSAFIRISHA SILAHA KWA MEXICO

Marekani imewafungulia mashtaka rasmi dhidi ya raia kadhaa wa kimataifa, akiwemo raia mmoja wa Uganda, kwa madai ya kushiriki njama ya kusafirisha silaha hatari za kijeshi kwa moja ya magenge ya uhalifu yanayojulikana kwa ukatili duniani.

Peter Dimitrov Mirchev, Michael Katungi pamoja na raia wa Kenya Elisha Odhiambo Asumo na wa Tanzania Subiro Osmund Mwapinga wanadaiwa kushirikiana kusambaza silaha za kijeshi kwa njia ya kimagendo na kuwauzia magenge ya Mexico hasa CJNG.

Silaha hizo ni pamoja na kijibomu, vifaa vya kurusha makombora , bunduki za kugundua umbali mrefu, mabomu yakutega ardhini na silaha za kupambana na ndege za kivita.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Wilaya ya Mashariki ya Virginia, watuhumiwa hao wanadaiwa kupanga na kupata kwa njia ya udanganyifu cheti cha mtumiaji wa mwisho (End User Certificate – EUC) kutoka kwa taifa lingine ambalo ni Tanzania ili kuficha nia halisi ya mahali silaha hizo zingeelekezwa.

Kwa kutumia cheti hicho, silaha 50 za kivita aina ya AK-47, pamoja na magazini na risasi, zilisafirishwa kutoka Bulgaria katika kile kilichoelezwa kuwa “mzigo wa majaribio.”

Ingawa nyaraka zilionesha kuwa zilikusudiwa kutumiwa nchini Tanzania, uchunguzi umebaini kuwa zilikuwa zikitumwa kwa CJNG (Cartel de Jalisco Nueva Generación) genge lenye historia ya ghasia, mauaji, na biashara haramu ya dawa za kulevya huko Mexico.

Aidha inadaiwa kuwa CJNG ilikuwa ikinuia kutumia silaga hizo katika usafirishaji wa dawa za kulevya kwa njia ya meli kuingia Marekani.

Mwezi Februari mwaka huu CJNG iliwekwa kama kikundi cha kigaidi kupitia amri ya kiutendaji ya 13224. Uuzaji wa silaha kwa magenge kama vile CJNG ni marufuku nchi zote.

Kesi hiyo inachunguzwa kwa kina na kitengo maalum cha operesheni za Shirika la Kukabiliana na Dawa za Kulevya (DEA) kupitia Kitengo cha Uchunguzi wa Pande Mbili, kwa ushirikiano mkubwa kutoka jeshi la polisi la kitaifa la Ugiriki.

Kwa mujibu wa maelezo ya wizara ya sheria ya Marekani, uchunguzi huu ni sehemu ya mpango mkubwa wa taifa uitwao “Operation Take Back America” kampeni inayolenga kukabiliana na uhamiaji haramu, kusambaratisha kabisa magenge ya dawa za kulevya na mitandao ya uhalifu wa kimataifa, pamoja na kuwalinda raia wa kawaida dhidi ya athari za uhalifu wa kutumia nguvu.

Ni muhimu kufahamu kuwa hadi sasa, haya yote ni tuhuma. Kwa mujibu wa sheria, mtuhumiwa huchukuliwa kuwa hana hatia hadi atakapopatikana na hatia mahakamani.

 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI