Header Ads Widget

KALENGA INAHITAJI MTU SAHIHI WA KUTUMWA AMBAYE NI MIMI – GRACE TENDEGA

 


Na Matukio Daima Media , Kalenga

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kalenga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Grace Victor Tendega, amesema wakati umefika kwa wananchi wa Kalenga kumchagua mtu sahihi wa kuwatumikia, mtu anayejua namna ya kuchukua kero za wananchi, kuzipeleka sehemu husika na kurudi na majibu yenye tija. 


Akizungumza na wananchi katika moja ya mikutano yake ya kampeni, Tendega amesema kuwa yeye ndiye mtu huyo sahihi anayefaa kupewa dhamana ya kulitumikia jimbo hilo kwa uaminifu na uwajibikaji wa kweli.

“Kalenga ina kila kitu – ardhi nzuri, watu wachapakazi, mito ya kutosha – lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa uwakilishi makini. Tunahitaji mtu anayeweza kuzungumza kwa sauti ya wananchi bungeni, sio mtu wa kushika nafasi kwa majigambo na kujisifu, halafu matatizo ya wananchi yakabaki pale pale,” alisema Tendega.

Akitolea mfano wa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, licha ya Kalenga kuwa na mito mingi inayoweza kuchimbwa visima au kufungwa miradi ya maji ya bomba, Tendega alisema hilo linaashiria wazi kuwa tatizo haliko kwenye uwezo wa serikali bali liko kwenye usimamizi na uwakilishi hafifu wa maeneo husika. 


Alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa ya maji kila kona ya nchi, hivyo haiwezekani Kalenga ikose miradi kama hiyo kama kero za wananchi zingechukuliwa kwa uzito unaostahili.

“Leo hii kuna vijiji Kalenga bado wanatembea zaidi ya kilomita kupata maji, wakati serikali yetu kila mwaka inaongeza bajeti ya miradi ya maji tatizo ni kwamba watu waliopata nafasi ya kuwawakilisha wananchi hawafiki kusikiliza kero halisi, bali wanapeleka maoni yao binafsi bungeni,” alisema.

Tendega alisisitiza kuwa yeye ni mkazi halisi wa Kalenga, na hata alipokuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chadema, alikuwa anaishi Kalenga na kushuhudia maisha ya kila siku ya wananchi wenzake. 


Alisema tofauti ya sasa ni kuwa, wakati akiwa Chadema alikumbwa na ugumu wa kupeleka hoja za maendeleo kutokana na ukosefu wa msimamo wa maendeleo wa chama hicho. Ndiyo maana, baada ya kutafakari kwa kina, aliamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi ambacho kina dira na sera za maendeleo.

“Wakati niko Chadema, nilikuwa na ndoto kubwa ya kuwatumikia wananchi wa Kalenga, lakini mazingira ya chama hayakuwa rafiki. Nilihitaji chama chenye dira ya kweli ya maendeleo, chama kinachosikiliza wananchi na kuwajali, ndipo nikajua CCM ndiyo mahali sahihi pa kuendeleza harakati za kweli za maendeleo ya wananchi,” alisema kwa msisitizo.

Aliwaomba wananchi wa Kalenga kumpa ridhaa ya kuwa Mbunge wao, akiahidi kuwa hatakuwa Mbunge wa kutoka mjini kwenda kijijini kwa msimu tu wa siasa, bali atakuwa Mbunge mkazi ambaye anajua shida za wananchi wake na atakuwa karibu nao muda wote. 


Aliahidi kuwa akichaguliwa, atapambana kuhakikisha kuwa kila kijiji kinapata huduma bora za msingi ikiwemo maji safi, elimu bora, huduma za afya na miundombinu ya barabara inayopitika majira yote ya mwaka.

“Najua tatizo la barabara Kalenga linavyochangia kudhoofisha uchumi wa wananchi wetu Mimi si muonaji bali ni mshiriki wa maisha ya kila siku ya Kalenga, najua namna bodaboda wanavyopata tabu, najua namna mama anavyoshindwa kufika kliniki kwa sababu ya barabara mbovu. Sitaki kuja kusimulia tu matatizo haya, nataka kupewa nafasi ya kuyashughulikia kwa nguvu zote,” alisema.

Kwa kumalizia, Tendega aliwahimiza wananchi wa Kalenga kuwa makini katika kuchagua viongozi mwaka huu, wakizingatia historia ya mgombea, uwezo wake wa kuchapa kazi, ukaribu wake na wananchi, pamoja na msimamo wake wa kisera. Alisema kwamba Kalenga siyo sehemu ya majaribio ya uongozi bali inahitaji mtu tayari ambaye ana maono na uwezo wa kutekeleza mipango ya maendeleo.

“Sitaki niwe mbunge wa kusifiwa mjini, nataka niwe mbunge wa kutenda kazi Kalenga naomba kura zenu, naahidi sitawaangusha,” 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI