Header Ads Widget

DIT WAPONGEZWA KWA WELEDI NA KASI UTEKELEZAJI WA MRADI WA EASTRIP

 Na Mwandishi Wetu .

Dar es Salaam, Tanzania — Wajumbe wa Baraza la Vyuo Vikuu vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (IUCEA) wameonyesha kuridhishwa kwa kiwango cha juu na maendeleo ya haraka na yenye ubora yaliyofikiwa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) chini ya mradi wa EASTRIP – yaani East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project.


Katika ziara yao rasmi iliyoambatana na ukaguzi wa miundombinu ya mradi huo, wajumbe hao walishuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa ujenzi wa Kituo cha Umahiri wa TEHAMA (ICT Centre of Excellence) pamoja na mabweni ya kisasa kwa ajili ya wanafunzi. Kwa sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia takribani asilimia 98, jambo ambalo limewavutia na kuwafanya wajumbe hao kutoa pongezi za dhati kwa DIT.




DIT imeendelea kuwa kielelezo cha mafanikio katika utoaji wa elimu ya ufundi stadi na teknolojia, si tu kwa Tanzania bali kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Kupitia mradi huo mkubwa unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (World Bank), DIT imedhihirisha uwezo wake wa kiutawala, kitaaluma na kiutekelezaji kwa kiwango kinachovutia.

Kituo hiki kipya cha umahiri kitakuwa na nafasi ya kutoa mafunzo ya kisasa ya TEHAMA kwa wanafunzi wa ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi katika sekta ya teknolojia na mawasiliano, ambayo ni injini ya maendeleo ya kisasa. DIT inaamini kuwa TEHAMA ni msingi wa mageuzi ya viwanda na kwa hilo, taasisi hiyo imejikita kuibadilisha jamii kupitia elimu bora yenye maarifa ya kisasa.




Majengo ya kituo hicho yamebuniwa kwa viwango vya kimataifa – yakiwa na maabara za kisasa, madarasa ya kisasa ya kidigitali pamoja na mifumo ya kiteknolojia inayowezesha ufundishaji kwa njia ya ana kwa ana na mtandaoni (blended learning). Pia mabweni yaliyokamilika yana uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya wanafunzi wa ndani na nje ya nchi, hivyo kukuza mtangamano wa kikanda kupitia elimu.

Katika hotuba ya mwakilishi wa wajumbe hao kutoka IUCEA, alisisitiza kuwa DIT imekuwa mfano wa kuigwa kwa maendeleo makubwa na ufanisi usio wa kawaida. DIT imeonyesha dhamira ya kweli katika kukuza elimu ya ufundi na teknolojia. Mradi huo umebuniwa kwa weledi na utekelezaji wake umevuka matarajio.

Kupitia EASTRIP, DIT haitakuwa tu na jukumu la kitaifa bali pia kituo kikuu cha mafunzo ya kikanda ambapo wanafunzi kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na nchi nyingine wataweza kujiunga kwa ajili ya kupata mafunzo ya kiwango cha juu kwenye sekta ya TEHAMA.

Mradi huo pia umefungua milango kwa fursa za ajira, utafiti wa pamoja, ubunifu wa kiteknolojia na ubadilishanaji wa wataalamu kati ya vyuo mbalimbali vya ukanda huu wa Afrika Mashariki.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI