Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
BENKI ya Ushirika Tanzania (Coop Bank) imetangaza kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Nanenane 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, ikiwa ni miongoni mwa wadhamini wa maonesho hayo makubwa ya kilimo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la benki hiyo Agosti 1, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank, Bw. Godfrey Ng’urah, amesema benki hiyo imejikita katika kuihudumia sekta ya kilimo kwa vitendo, huku ikilenga kutoa huduma bora za kifedha kwa wakulima, vijana na wajasiriamali katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo-biashara.
“Coop Bank ni benki namba moja ya ushirika nchini. Wamiliki wake wakuu ni vyama vya ushirika vinavyomilika zaidi ya asilimia 51 ya benki – hii ni benki ya wakulima. Soko letu kuu lipo kwenye sekta ya kilimo, ndiyo maana tumeliona jambo hili la Nanenane kuwa la muhimu sana kwetu,” alisema Bw. Ng’urah.
Alibainisha kuwa mazao yote ya kimkakati kama vile kahawa, korosho, chai, ufuta, mbahazi na mengineyo yanapitia katika mifumo ya vyama vya ushirika (AMCOS na UNION), ambao ndio wateja wakuu na wamiliki wa benki hiyo. Coop Bank inatoa huduma za kifedha zinazolenga kusaidia ukusanyaji, usindikaji, masoko na uuzaji wa mazao hayo ndani na nje ya nchi.
“Tuna vyama vikuu vya ushirika kote nchini vinavyosimamia mifumo ya mauzo ya mazao ya wakulima. Hii ndiyo benki pekee inayomilikiwa na wanachama wa ushirika. Wakulima mmoja mmoja, AMCOS na UNION zote ni sehemu ya benki hii,” alieleza.
Bw. Ng’urah pia alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi kuwa benki hiyo ilianza rasmi shughuli zake mwezi Oktoba mwaka jana na kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Aprili mwaka huu. Kwa sasa, Coop Bank ina matawi katika mikoa mitano: Kilimanjaro, Tabora, Moshi, Mtwara na Dodoma ambayo ni makao makuu.
“Tunawakaribisha wakulima, wafanyabiashara, vijana, wanawake na wadau wote wa kilimo kutembelea banda letu hapa katika eneo la wadhamini wakuu, na pia banda la Kijiji cha Ushirika. Katika mabanda haya mawili, tutakuwa tunatoa elimu, huduma na bidhaa zetu za kifedha kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya kilimo,” aliongeza.
Maonesho ya Nanenane mwaka huu yamefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, yakibeba kaulimbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.”
0 Comments