Na Hamida Ramadhan,MatukioDaima Media Dodoma
WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe, ameiagiza rasmi Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kuhakikisha inawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote wanaojihusisha na uuzaji wa mbegu bandia nchini.
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya TOSCI, Waziri Bashe amesema biashara ya mbegu feki imekuwa kikwazo kikubwa kwa wakulima, na hivyo kunahitajika hatua kali za kisheria kuchukuliwa ili kukabiliana na changamoto hiyo.
“Hii ni vita tunahitaji TOSCI isimame imara, ifanye ukaguzi wa mara kwa mara sokoni, iwakamate wanaovunja sheria na kuhakikisha wanashitakiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo. Mbegu bandia ni janga kwa maendeleo ya kilimo nchini,” alisema Bashe.
Kwa upande Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI Nyasebwa Chimagu alieleza kuwa taasisi hiyo inaendelea na uwekezaji mkubwa katika mifumo ya ukaguzi, uchunguzi na ufuatiliaji wa ubora wa mbegu, ili kuhakikisha kila mbegu inayofika kwa mkulima ni bora na imehakikiwa.
“Tunaendelea na uwekezaji kwenye teknolojia na rasilimali watu. Tutafika kila kona ya nchi kushirikiana na serikali na wadau wengine ili kuzuia mbegu zisizo na viwango kuingia sokoni,” alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha, mjadala umeibuka kuhusu umuhimu wa kulinda mbegu za nasaba au asili, ambazo zinaweza kusaidia wakulima kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Wadau wameeleza kuwa mbegu hizi zimekuwa zikivumilia hali ngumu ya mazingira na zinapaswa kuhifadhiwa na kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
“Tayari kuna aina kadhaa za mbegu za asili ambazo zimetambuliwa rasmi. Kinachohitajika sasa ni mikakati madhubuti ya kuzihifadhi, kuzifanyia utafiti na kuziwezesha kushindana na mbegu zilizosindikwa kibiashara,” alisema mmoja wa wataalamu wa kilimo aliyeshiriki hafla hiyo.
Uzinduzi wa Bodi mpya ya TOSCI unatajwa kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi wa sekta ya mbegu nchini, hasa katika kipindi hiki ambacho kilimo kinahitaji mageuzi ya haraka ili kuendana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na mahitaji ya soko.
0 Comments