Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu Mwamba, amehimiza uandaaji wa mipango na bajeti unaozingatia vipaumbele vya kisekta, kitaasisi na kitaifa ili kuepuka matumizi yasiyo ya lazima na kuhakikisha uwiano wa matumizi ya fedha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kikao kazi cha kitaifa cha wataalam wa bajeti na mifumo ya fedha serikalini, kinachofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Jengo la Treasury Square jijini Dodoma Dkt. Mwamba amesisitiza kuwa mafanikio ya bajeti yoyote yanategemea mipango thabiti, usimamizi madhubuti na utekelezaji unaolenga vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
Kikao kazi hicho kimewaleta pamoja wataalam kutoka Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25, kuandaa bajeti ya mwaka 2025/26 na kukusanya maoni kwa ajili ya Mwongozo wa Uandaaji wa Mpango na Bajeti wa mwaka 2026/27.“Tunalo jukumu la kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi mkubwa, tukizingatia miongozo ya kitaifa kama Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), na Waraka wa Hazina Na. 1 wa mwaka 2025/26,” amesema Dkt. Mwamba.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa washiriki kutumia fursa ya kikao kazi hicho kubadilishana uzoefu, kutoa ushauri wa kitaalamu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha mchakato mzima wa bajeti.
Vilevile, ametoa pongezi kwa mashirika ya maendeleo, vyuo vikuu na wataalamu wa ndani kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa bajeti ikiwemo CBMS na MUSE.
Dkt. Mwamba amewataka washiriki kushiriki kikamilifu katika mijadala na mafunzo yanayoendelea, ili kuhakikisha kuwa matokeo ya kikao kazi hicho yanakuwa na mchango wa kweli katika ufanisi wa upangaji na utekelezaji wa bajeti za serikali kwa maendeleo ya wananchi.
0 Comments