Mkutano huo mkubwa unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa ya Afrika na visiwa vya Karibiani una kaulimbiu inayosema: “Uhimilivu na Mabadiliko: Kuimarisha Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Afrika na Karibiani katika Kipindi cha Changamoto za Kidunia.”
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu anatarajiwa kushiriki mjadala wa Mjadala wa Wakuu wa Nchi na Serikali, kukutana na viongozi wa mataifa mengine, pamoja na kushiriki katika mikutano ya uwili na wawekezaji wakubwa, ikiwa ni dhamira ya Tanzania ya kuendeleza juhudi zake za kuvutia wawekezaji wa kimataifa ili kusaidia katika kujenga uchumi wa kisasa na shindani duniani.
Ushiriki wa Mheshimiwa Majaliwa katika mkutano huo akimwakilisha Rais Dkt. Samia ni mwendelezo wa dhamira ya dhati ya kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuifungua nchi kimataifa na kuimarisha ushirikiano, ili kuchochea maendeleo jumuishi kwa Watanzania wote.
Baadhi ya maeneo muhimu ambayo yatajadiliwa katika mkutano huo ni kuanzishwa kwa eneo la Biashara Huria kati ya Afrika na Karibiani, kuimarisha baraza la biashara la Afrika na Karibiani, kuchochea uchumi na ubunifu pamoja na Kukuza uhusiano wa usafiri wa anga na baharini kati ya Afrika na Karibiani.
Mkutano huo umeratibiwa na Jamhuri ya Granada pamoja na taasisi ya kifedha ya kimataifa yenye lengo la kukuza biashara ya bidhaa na huduma ndani na nje ya Afrika (Afreximbank).
0 Comments