WATU wenye ulemavu nchini wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha wanawashirikisha kikamilifu katika mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo imezinduliwa rasmi leo Julai 17, 2025 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wakizungumza baada ya uzinduzi huo, watu wenye ulemavu wamesema dira hiyo inagusa na kujibu changamoto zao nyingi, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa elimu jumuishi, huduma bora za afya, miundombinu rafiki, fursa za ajira na ushiriki katika nafasi za uongozi.
Akizungumza kwa niaba ya jamii hiyo, Maiko Salali, Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Disabilities Hope (FDH), alisema Dira hiyo ni ya kihistoria kwa watu wenye ulemavu, kwani kwa mara ya kwanza mchakato mzima ulikuwa jumuishi na shirikishi, hali iliyowawezesha kutoa maoni yao moja kwa moja.
“Tunapongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kutusikiliza. Dira hii si tu inatutambua, bali pia inaelekeza wazi nini kifanyike ili kutatua changamoto zetu," Amesema
Na kuongeza "Sasa ni wakati wa sisi wenyewe kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake,” amesema Salali.
Salali amesisitiza kuwa Dira hiyo ni fursa ya kipekee ya kuhakikisha watu wenye ulemavu hawabaki nyuma katika safari ya maendeleo ya taifa, na kwamba usimamizi wa utekelezaji wake unapaswa kuwajumuisha wadau wote, wakiwemo viongozi wa Serikali, mashirika ya kiraia, na sekta binafsi.
0 Comments