Header Ads Widget

WATAALAMU WA RASILIMALI WATU WAHIMIZWA KUJIUNGA NA JUMUIYA ZA KITAALUMA

 


Na Pamela Mollel, Arusha

Waajiri kote nchini wametakiwa kuzingatia maelekezo ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu namna bora ya ushiriki wa watumishi katika mikutano ya jumuiya zinazotambuliwa rasmi na serikali, zikiwemo jumuiya za kitaaluma kama TAPAHR. 

Ushiriki huo umetajwa kuwa nyenzo muhimu ya kuongeza weledi, kujenga mitandao ya kitaalamu, na kuimarisha utendaji katika utumishi wa umma.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, alipokuwa akihutubia katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Jumuiya ya Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala katika Utumishi wa Umma (TAPAHR) unaofanyika mkoani Arusha.

Mhandisi Zena amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wataalamu wa kada hiyo kujiunga na TAPAHR ili waweze kunufaika na fursa za mafunzo, kubadilishana uzoefu, na kujengewa uwezo wa kuongeza ufanisi kazini.


Aidha, amewataka wanachama wa jumuiya hiyo kujiepusha na tabia za uchu wa madaraka na ubadhirifu wa fedha ili kuepusha migogoro na kuyumbisha mwelekeo wa jumuiya.



“Tunataka TAPAHR iwe mfano wa jumuiya yenye nidhamu, maadili na dira ya maendeleo kwa kada ya rasilimali watu. Tusikubali kufanya mambo yanayokinzana na malengo ya kuanzishwa kwake,” alisema Mhandisi Zena.


Katika kuhakikisha taaluma hiyo inaimarika zaidi, Mhandisi Zena pia ametoa wito kwa viongozi wa TAPAHR kuanza mchakato wa kuanzisha Bodi ya Kitaaluma itakayoratibu na kusimamia maendeleo ya wataalamu wa kada hiyo nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi, amewahimiza wataalamu hao kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika taasisi zao kwa kuzingatia maadili ya kazi, uwajibikaji na ubunifu katika utumishi wa umma.


Naye Mwenyekiti wa TAPAHR, Bi. Grace Meshy, amesema kuwa jumuiya hiyo ilianza rasmi kutekeleza majukumu yake mwaka 2024 kwa lengo la kuwaunganisha wataalamu wa kada hiyo, kuongeza ushirikiano, na kusukuma mbele ajenda ya maboresho katika utumishi wa umma.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI