Header Ads Widget

WADAU WAHIMIZA UTAFITI NA TATHMINI YA MAFANIKIO NA CHANGAMOTO ZA MIRADI YA UBIA NCHINI

Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Serikali, Prof. Adelardus Kilangi,

Na chausiku said 

Matukio Daima Media Mwanza.

Wadau wa maendeleo nchini wamependekeza kufanyika kwa tathmini ya kina juu ya mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) ili kusaidia kuboresha mwelekeo mpya wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Wito huo umetolewa Julai 26, 2025 katika kongamano lililofanyika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT) jijini Mwanza, likiwa na lengo la kuchambua nafasi ya PPP katika kufanikisha malengo ya kiuchumi ya taifa, yakiwemo kuongeza Pato la Taifa hadi kufikia dola trilioni moja kufikia mwaka 2050.

Miongoni mwa waliotoa wito huo ni Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Serikali, Prof. Adelardus Kilangi, ambaye alisisitiza umuhimu wa kufanya uchambuzi wa historia ya utekelezaji wa PPP nchini, ili kujifunza kutokana na makosa yaliyopita na kuboresha mfumo wa sasa.

 “Ipo haja ya kufanya uchambuzi mpana wa historia ya PPP nchini. Tusijifunge tu kwenye sheria ya PPP pekee, bali tuangalie mfumo mzima wa kisheria na kiutendaji ulioathiri mafanikio au kushindwa kwa baadhi ya miradi,” alisema Prof. Kilangi.


Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa PPPC, David Kafulila, alisema Tanzania inalenga kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa duniani, ikiwa ni pamoja na kufikia Pato la Taifa la dola trilioni moja na wastani wa dola 7,000 kwa kila Mtanzania ifikapo mwaka 2050.

“Haya ni malengo makubwa lakini yanawezekana. Tayari nchi imeweka mazingira bora ya kisera na kisheria kuimarisha PPP, lakini pia tunahitaji kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi,” alisema Kafulila.

Kwa mujibu wa Prof. Kilangi, tafiti za kihistoria na kisera zinaweza kusaidia serikali na wadau kubuni njia bora na za kidemokrasia za kushirikiana kwenye miradi ya maendeleo – bila kurudia makosa ya nyuma kama ya mikataba isiyo na uwazi au usimamizi hafifu.

Dkt. Delphine Kessy kutoka SAUT naye alipendekeza kuanzishwa kwa chombo huru kitakachofanya tafiti, kuishauri PPPC na kusaidia kufuatilia utekelezaji wa miradi kwa uwazi na tija.

“Chombo hicho kiwe na mamlaka ya kutoa mrejesho kwa umma na kusaidia kuweka viwango vya kitaifa vya utekelezaji wa PPP. Hii itasaidia sana kuelekea mafanikio ya Dira ya 2050,” alisema Dkt. Kessy.


Aidha, Dkt. Jasinta Msamula alisisitiza kuwa ufanisi wa PPP unahitaji mabadiliko ya kimfumo kwenye bajeti na usimamizi wa serikali za mitaa, huku akitaka tafiti za kisayansi zipewe nafasi kubwa katika kuongoza maamuzi ya kisera.

Kongamano hilo liliwakutanisha wataalamu, wanazuoni, viongozi wa taasisi za umma na binafsi pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu, ambao walihimiza kuwepo kwa mfumo wa kisheria unaotabirika, uwazi katika mikataba, pamoja na ushirikishwaji wa jamii katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI