Header Ads Widget

UIMBAJI WA INJILI WATAJWA KUWA NGUZO YA AMANI NA MAENDELEO KWA JAMII.

Na Lilian Kasenene,Kilombero

Matukio DaimaApp 

UINJILISHAJI kupitia nyimbo za Injili umetajwa kuwa mojawapo ya njia zinazoweza kusaidia kujenga Taifa lenye maadili, mshikamano na utulivu wa kudumu, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia changamoto nyingi za kimaadili, kiuchumi na kijamii.

Kauli hiyo imetolewa na Bi Idda Mushi, Mwandishi wa Habari Mwandamizi, wakati akihutubia waumini na wageni waliofika katika Kanisa la Anglikana la K1 Ruaha la Dayosisi ya Morogoro, lililopo wilayani Kilombero, Mkoani Morogoro kwaajili ya hafla ya uzinduzi wa albamu ya nyimbo za Injili ya muimbaji Anna Syprian Ngalupela ya "Wastahili Bwana".

Alisema kuwa muziki wa Injili sio tu burudani, bali ni huduma ya kiroho ambayo ikitumiwa vizuri inaweza kuwa mkombozi wa nafsi za watu, chanzo cha matumaini kwa waliovunjika moyo, na njia ya kukuza mshikamano miongoni mwa Watanzania wa dini zote.

Katika hotuba yake, Idda alihimiza jamii kuwekeza kwenye vipawa vya vijana wanaochagua kumtumikia Mungu kwa njia ya nyimbo na kutoa wito kwa wadau kumsaidia mwimbaji Anna kufanikisha ndoto yake ya kurekodi nyimbo za kuabudu kwa mfumo wa “live worship” kama sehemu ya uamsho wa kizazi kipya cha waimbaji wa Injili.

Katika tukio hilo lililohudhuriwa na waumini na wageni mbalimbali, Anna alieleza jinsi alivyoanza huduma ya uimbaji tangu mwaka 2008, na sasa amefanikisha kurekodi albamu yake ya kwanza ya video kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 3.5, bila msaada wowote wa moja kwa moja kutoka kwa mfadhili.

Kwa kuguswa na juhudi zake, Bi Idda Mushi kwa niaba ya Wakili Elizabeth Mwase aliyewakilishwa katika hafla hiyo kama mgeni rasmi waliahidi kuchangia shilingi milioni moja na laki tano (1,500,000/-),shilingi laki tano zikitolewa fedha taslimu kusaidia jitihada hizi.

"Huduma  hii ya Uinjilishaji kwa njia ya nyimbo inayofanywa na Anna ni huduma ya ushindi, faraja na uponyaji wa roho. Tunapaswa kuiunga mkono kwa moyo, kwani kwa kufanya hivi nasi tutakuwa sehemu ya kusaidia kuponya jamii inayokabiliana na changamoto mbalimbali za maisha ikiwemo mmomonyoko wa maadili" alisema Idda.

Akisoma risala yake muimbaji Anna  Ngalupela alisema alianza huduma ya uimbaji Mwaka 2008 na alitumika sehemu mbalimbali kwenye mikutano ya injili na semina za nenonla Mungu Hadi Mwaka 2019 alipofanikiwa kurekodi albamu yake ya kwanza ya audio.

Anna alisema "Maono yangu ya mbele ni kufikiria kurekodi live nyimbo za kusifu na kuabudu ambapo gharama yake ni kubwa na inahitaji maandalizi makubwa ya kutosha,".

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI