Na Fadhili Abdallah,Kigoma
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa Kigoma imesema kuwa inazo mbinu na vyanzo vipya vya kupata taarifa ili kuweza kudhibiti vitendo vya rushwa katika michakato mbalimbali ya uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Afisa Dawati la elimu kwa umma TAKUKURU mkoa Kigoma, Abecha Bakari alisema hayo katika kikao kazi na waandishi wa habari kuweka mpango wa pamoja wa ushirikiano katika kufanya kazi wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu.
Bila kutaja mbinu hizo alisema kuwa pamoja na mambo mengine wameongeza pia vyanzo vya taarifa na namna ya kupata taarifa hizo na kuzifanyia kazi hivyo wanauhakika kuwa mwaka huu udhibiti wa vitendo vya utoaji na upokeaji rushwa utadhibitiwa.
Akizungumza katika kikao kazi hicho Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma, John Mgallah aliomba ushirikiano kutoka kwa waandishi wa habari mkoani Kigoma kutumia vyombo vyao vya habari kutoa elimu kwa umma kupitia vipindi mbalimbali kueleza madhara ya kuchagua viongozi kwa misingi ya kupewa rushwa.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Chama Cha waandishi wa habari mkoa Kigoma, Jacob Ruvilo alisema kuwa waandishi wa habari wako tayari kufanya kazi na TAKUKURU na kwamba wameomba taasisi hiyo kutoa ushirikiano hasa taarifa za matukio ya wagombea wanaokamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.
0 Comments