-Mtaka atoa maneno mazito kuhusu chokochoko na ugomvi.
Na Mwandishi Wetu, Mbozi.
MADIWANI wa Viti Maalum, Neema Mwandabila na Juliana Shonza, wametetea kwa kishindo nafasi zao za ubunge wa viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe, katika uchaguzi uliofanyika Julai 31, 2025.
Uchaguzi huo uliosimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kanisa la Moravian mjini Vwawa, wilayani Mbozi, ambapo wagombea tisa walichuana kuwania nafasi hizo mbili.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Mtaka, jumla ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo walikuwa 739 ambapo kura tano ziliharibika.
Shonza aliibuka kinara kwa kupata kura 572 akifuatiwa na Mwandabila aliyepata kura 356.
Wagombea wengine waliopata kura ni pamoja na Tuli Magila (167), Tumaini Mbembela (122), Shukurani Mkondya (86), Winfrida Shonde (56), Mesia Swella (44), Betha Minga (34) na Neema Lwila (29).
Akizungumza kabla ya kutangaza matokeo, Mtaka aliwashukuru Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Taifa kwa imani waliyoionesha kwake kwa kumteua kuwa msimamizi wa uchaguzi huo Mkoani Songwe.
Pia aliwapongeza wajumbe wa mkutano mkuu kwa ukomavu wa kisiasa na nidhamu waliyoionyesha hadi kufanikisha zoezi hilo kwa amani na utulivu.
Mtaka aliwapongeza wagombea wote walioshinda na waliopata kura chache, akisisitiza kuwa kushiriki ni hatua kubwa ya uongozi na kila mmoja ameonesha nia ya kuwatumikia wananchi.
Hata hivyo, Mtaka hakuacha kutoa nasaha nzito kwa washindi, akiwataka kuwa waangalifu na kujiepusha na chokochoko zisizo na msingi kabla ya vikao vya mwisho vya uteuzi.
Akiwasihi Shonza na Mwandabila kuishi kwa upendo na mshikamani kwenye mfumo wa maisha kuna kesho ndefu na pia maisha yana fumbo kubwa.
"Kama mlikuwa na chokochoko au kugombanishwa na wapambe, tafadhali achaeni maana hakuna mtu anayejua kesho wala keshokutwa yake” alisisitiza Mtaka.
Kwa wale ambao kura hazikutosha, Mtaka aliwatia moyo na kuwataka kuendelea kushiriki katika jitihada za maendeleo ya Mkoa wa Songwe.
0 Comments