Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Balozi Simon Siro amewataka watumishi wa umma mkoani Kigoma kutokuwa kikwazo katika kusimamia kwa vitendo mpango wa serikali wa kuufanya mkoa Kigoma kuwa mkoa wa kimkakati kwa uchumi na biashara katika kutekeleza Diplomasia ya uchumi.
Akuzungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya Kasulu, watumishi wa halmashauri ya mji Kasulu, taasisi za serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa watumishi wa uuma wana mchango mkubwa katika kutekeleza na kusimamia kwa vitendo utekelezaji wa diplomasia ya uchumi mkoani humo.
Kutokana na hilo Balozi Siro ambaye yupo kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku nne mkoani Kigoma alisema kuwa watumishi wa umma wilayani Kasulu wanapaswa kufanya kazi na kuwajibika kikamilifu ili kutimiza mpango wa serikali wa utekelezaji wa Diplomasia ya uchumi mkoani Kigoma.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa kutekeleza mpango wa kuufanya mkoa Kigoma kuwa mkoa kimkakati kiuchumi na biashara kunahitaji uwajibiki wa kila mdau hivyo watumishi wa umma mkoani humo wanalo jukumu na wajibu mkubwa katika kushiriki kwenye jambo hilo kikamilifu.
Kutokana na hilo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa mkoa unavyo vipaumbele hivyo watumishi wanapaswa kufanya kazi kulingana na vipaumbele hivyo ikiwemo kusimamia kwa karibu masuala ya uchumi na biashara sambamba na kuhakikisha mikopo ya halmashauri ya asilimia 10 inatolewa na kuwafikia walengwa.
Awali akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa wilaya Kasulu, Kanali Isack Mwakisu alisema kuwa wilaya ya Kasulu ni moja za wilaya za mkoa Kigoma ambayo inatambulika kama wilaya ya kimkakati kiuchumi hasa kwa soko la nchi za ukanda wa maziwa makuu na hivyo inasimamia kwa karibu mipango yake kuelekea diplomasia ya uchumi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa katika kuhakikisha wanatekeleza hilo wanasimamia kwa karibu masuala ya ulinzi na usalama ili suala hilo lisiweze kuvuruga Amani ya wilaya hiyo na kushindwa kutekeleza mpango mkakati wao wa kutekeleza masuala ya Diplomasia ya uchumi.
Mwisho.
0 Comments