Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amesema mkoa umeanzisha ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Shirika la Biashara la Zanzibar (ZSTC) ili kuongeza uzalishaji wenye tija wa mazao ya viungo, yakiwemo mdalasini, iliki, karafuu na pilipili manga.
Ameyasema hayo leo Julai 15 ,2025 jijini hapa wakati akieleza mafanikio ya serikali ya miaka minne ambapo amesema ,mpango huo unalenga kuimarisha viwanda vya usindikaji na kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi kwa wakulima wa viungo.
“Kwa sasa, mkoa wetu unazalisha tani 4,016 za viungo kwa mwaka, ambazo huingiza takribani shilingi bilioni 42.1. Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza tija, ajira, na mapato kwa wananchi wetu,” alisema Dkt. Burian.
Ametoa wito kwa wakulima kuongeza uzalishaji kwa kufuata kanuni bora za kilimo na kutumia fursa zinazotolewa kupitia ushirikiano huo.
Aidha amesema Mkoa wa Tanga umeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika uzalishaji wa mazao ya biashara, ukiwa kinara kitaifa kwenye baadhi ya mazao kutokana na mikakati ya ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.
Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amesema mkoa unazalisha zaidi ya asilimia 50 ya mkonge nchini, ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka tani 14,835 mwaka 2021 hadi kufikia tani 22,620 mwaka 2023. Mpango wa kuongeza viwanda vya usindikaji unaendelea kutekelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Katika zao la chai, mkoa unashirikiana na wawekezaji kuboresha miundombinu ya usindikaji na masoko. Uzalishaji wa chai kwa sasa ni tani 31,492, zenye thamani ya takribani shilingi bilioni 1.3.
Kwa upande wa korosho, mkoa umesambaza lita 22,890 za viuatilifu vya maji na tani 229.8 za sulphur zenye thamani ya shilingi bilioni 1.9, pamoja na mbegu bora za korosho kilo 5,943 zenye thamani ya shilingi milioni 29.7 kwa wakulima. Mashamba ya zamani yamefufuliwa kwa ekari 980. Kiasi cha kilo 366,966 za korosho ziliuzwa kupitia soko la bidhaa TMX, zikiiingiza shilingi milioni 925.9.
Katika zao la pamba, mkoa ulizalisha tani 1,200 zenye thamani ya shilingi bilioni 2.4, huku malengo yakiwa ni kufikia tani 2,500 ifikapo msimu wa mwaka 2029/30.
Zao la muhogo nalo limepewa kipaumbele, ambapo kwa sasa mkoa unazalisha tani 1,681,121, na lengo ni kufikia tani 2,256,150. Zao hilo linaingiza zaidi ya shilingi bilioni 16.8 kwa mwaka.
MWISHO.
0 Comments