Na Moses Ng’wat, Momba.
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Jabir Omar Makame, ametoa maelekezo kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuhakikisha ndani ya wiki moja wanawasilisha mpango kazi wa ununuzi wa mahindi ili kuwawezesha wakulima wa Mkoa huo kupata soko la uhakika kwa mazao yao.
Makame alitoa agizo hilo Julai 24, 2025, wakati wa ziara yake ya ukaguzi katika maghala sita ya mazao yaliyopo katika soko la Kimataifa la Kakozi, kijiji cha Kakozi, Kata ya Ndalambo, Wilayani Momba.
Alisema Serikali imejenga miundombinu wezeshi katika eneo hilo, na sasa ni wakati wa kuhakikisha soko hilo linatumika kikamilifu kuwaunganisha wakulima na wanunuzi wakubwa wa mazao, hususan mahindi.
"Tunahitaji kuhakikisha kwamba soko hili la Kakozi linakuwa kitovu cha biashara ya mazao yote kutoka maeneo ya jirani, hii itasaidia kukuza uchumi wa wakulima wetu na kuharakisha maendeleo ya Wilaya ya Momba kwa ujumla,” alisema Makame.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha soko la kimataifa la mazao Kakozi linakuwa kituo kikuu cha biashara ya mazao, hatua itakayovutia wafanyabiashara wakubwa, wa kati, na taasisi kama NFRA.
Aidha, Mwandobo alieleza kuwa ujenzi wa maghala hayo umeleta tija kubwa kwa kuchochea Halmashauri hiyo kupandisha uwezo wa kukusanya mapato ya ndani ya shilingi bilioni 3 katika mwaka wa fedha unaoisha, huku ikilenga kukusanya shilingi bilioni 4 katika mwaka wa fedha 2025/26.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kakozi, Amon Kayange, akizungumza kwa niaba ya wakulima, alisema licha ya changamoto za mvua, mavuno ya mwaka huu yamekuwa ya kuridhisha na wakulima wanasubiri kwa hamu Serikali itangaze rasmi ratiba ya ununuzi wa mahindi.
"Tuna mahindi mengi sana… matarajio yetu ni kwamba Serikali itanunua mazao haya kwa bei nzuri ili kuepusha hasara kwa wakulima,” alisema Kayange.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, Fabian Manoza, alisema kiasi cha shilingi 2,853,109,786 kimetumika kujenga maghala hayo sita katika soko hilo la kimataifa la mazao.
Manoza aliongeza kuwa maghala hayo huingizia Halmashauri hiyo kiasi cha shilingi 145,872,000 kwa mwaka kupitia wapangaji mbalimbali wakiwemo NFRA na kampuni ya LONG PING, hali inayoongeza mapato ya ndani ya Halmashauri.
0 Comments