Na Hamida Ramadhan, Mtukio Daima App Dodoma
SERIKALI ya Mkoa wa Kagera imejipanga kuendeleza kampeni maalum ya kuhamasisha wananchi kula mlo kamili kwa kutumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira yao, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kutokomeza tatizo la udumavu kwa watoto.
Kampeni hiyo inalenga kubadilisha mtazamo wa wananchi kuhusu lishe bora, ikiwahimiza kuachana na mazoea ya kula vyakula vya aina moja, hasa ndizi pekee, na badala yake kujumuisha makundi yote ya chakula katika mlo wa kila siku.
Akizungumza na waandishi wa habari Juu ya mafanikio ya awamu ya sita, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajati Fatma Mwasa, alisema mkoa huo una rasilimali nyingi za chakula zikiwemo samaki, maharage, mboga za majani, matunda na vyakula vingine vyenye virutubisho, lakini bado sehemu kubwa ya jamii imekuwa haitumii ipasavyo vyakula hivyo.
“Tumegundua kuwa pamoja na wananchi kulima na kuvua vyakula vya aina mbalimbali, bado wengi wanashikilia utamaduni wa kula ndizi kama chakula kikuu na kuacha vyakula vingine muhimu kwa afya. Hii imechangia kiwango kikubwa cha udumavu kwa watoto mkoani Kagera,” alisema Hajati Mwasa.
Aliongeza kuwa kama sehemu ya kampeni hiyo, serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wataalamu wa afya na lishe imeanza kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kula mlo kamili, kupika mapishi ya vyakula mchanganyiko, pamoja na matumizi ya virutubisho kwa watoto na mama wajawazito.
“Nikiwa kiongozi na pia mama, nimeona umuhimu wa kuwa karibu na jamii, kuwaelimisha juu ya ulaji bora. Tunawahamasisha wanawake kupika kwa ubunifu kwa kutumia vyakula walivyonavyo nyumbani ili watoto wapate lishe bora na kuondokana na udumavu,” alieleza.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kiwango cha udumavu kwa watoto mkoani Kagera kilikuwa asilimia 34.3, lakini kutokana na juhudi hizi, hali imeanza kubadilika na viwango vya udumavu vinaendelea kupungua.
Hata hivyo Serikali ya mkoa imesisitiza kuwa kila kaya ina uwezo wa kupata lishe bora endapo elimu ya lishe itazingatiwa, na mila potofu zinazozuia ulaji wa baadhi ya vyakula zitaachwa.
0 Comments