Na Seif Yustus, Arusha
MENEJIMENTI ya Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa mazingira Mkoa wa Arusha (AUWSA), imepongeza chama cha wafanyakazi wa viwanda, biashara, taasisi za fedha, huduma na ushauri (TUICO) Mkoa wa Arusha, kwa uamuzi wake wa kutoa mafunzo juu ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi WCF pamoja na mfuko wa hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wa umma (PSSSF), kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi rasilimali watu wa Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa mazingirs Jiji la Arusha (AUWSA), Kazimil Kanyanza aliwataka wafanyakazi kufuatilia kwa karibu mafunzo hayo ili kupata elimu sahihi kuhusiana na stahiki zao.
“Nyakati kama hizi za mafunzo ndio za kupata elimu sahihi kuhusiana na stahiki zako, lakini hata kujua zile fomula za kikokotoo, kuulizia mambo ambayo huyajui ili ujue na kujiandaa kuwekeza kabla ya kustaafu, isije ikatokea miaka miwili au mitatu baada ya kustaafu ukajikuta umetangulia mbele za haki kwa kuwa hukuwa umejiandaa,”amesema.
Aidha aliwataka wafanyakazi kutochagua viongozi wanaoenda kupambana na kuanzisha mgogoro na menejimenti badala yake wachague viongozi wenye ushawishi na uwezo wa kuwasilisha hoja zenye maslahi mapana kwa wafanyakazi ambazo zitakubalika na pande zote.
Hata hivyo amesema viongozi wa tawi la TUICO katika Mamlaka hiyo wamekuwa wakitekeleza majukumu yao vizuri kwa kuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya wafanyakazi ambao ni wanachama wao na kutoa wito kwa viongozi watakaochaguliwa kuiga mfano wa viongozi wanaomaliza muda wao.
Katibu wa TUICO Mkoa wa Arusha na Kanda ya Kaskazini, Joseph Patrick Shangali aliwataka watumishi ambao ni wanachama wa chama cha wafanyakazi TUICO kote nchini kutumia mafunzo ambayo wamekuwa wakipewa na watumishi wa TUICO kujua haki na stahiki zao wanazopaswa kuzipata kutoka kwa waajiri wao pamoja na kujiandaa vizuri kabla ya kustaafu.
Aidha ametoa wito kwa wafanyakazi vijana wanaopata ajira mpya kote nchini kujiunga na chama cha wafanyakazi TUICO ili kuweza kutetewa, kulindiwa haki na maslahi yao pindi wanapopatwa na madhila kazini kupitia kwa waajiri wao.
Shangali amesema chama hicho Mkoa wa Arusha kimeandaa mafunzo hayo kwa wafanyakazi wa AUWSA kwa lengo la kuwapa ufahamu kuhusu mfuko wa hifadhi ya jamii (PSSSF), pamoja na mfuko wa fidia (WCF) ili kuweza kujua stahiki zao pale wanapoumia kazini na baada ya kustaafu utumishi wa umma.
“ Wafanyakazi wengi wanafanyakazi katika mazingira hatarishi ya kupata ajali lakini hawapati stahiki zao kwa kuwa hawajui kama kuna mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF), ambao unapaswa kuwafidia wanapopata majanga kazini, hivyo leo tumewaletea maofisa kutoka WCF ili waeleze wafanyakazi hawa namna mfuko wao unavyofanyakazi,”amesema.
Amesema pia kumekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na kikokotoo hivyo wamelazimika kuwaita maofisa wa mfuko wa hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wa umma (PSSSF), kwa lengo la kutoa ufafanuzi masuala mbalimbali kuhusiana na mafao kwa wafanyakazi ikiwemo kikokotoo.
Shangali pia alisema viongozi wa TUICO katika mamlaka hiyo wamemaliza muda wao hivyo mbali ya mafunzo pia watasimamia uchaguzi ili kupata viongozi wapya watakaoongoza kwa miaka mingine mitano kama katiba ya TUICO inavyoelekeza.
0 Comments