NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kumteka na kumuua kikatili mchimbaji wa dhahabu, Nestory Marcel Inda (61), mkazi wa Stamico–Katoro, mkoani Geita, aliyeuawa kwa kunyongwa shingoni kisha mwili wake kutupwa ziwani katika eneo la Mwalo wa Ihale, wilayani Ilemela.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 14, 2025, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa, alisema kuwa mwili wa marehemu ulipatikana Juni 28, 2025, ziwani katika eneo la Mwalo wa Ihale, ukiwa umetupwa na kuonekana na wavuvi waliotoa taarifa kwa polisi.
“Mwili ulikuwa wa mwanaume mtu mzima, lakini hakuweza kutambulika mara moja. Baadaye tulibaini kuwa ni Nestory Marcel Inda, aliyeripotiwa kutoweka Geita tangu Juni 23 mwaka huu,” alisema Kamanda Mtafungwa.
Kamanda Mtafungwa aliwataja kwa majina watuhumiwa wanaohusishwa na tukio Hilo ni pamoja na Jacob Elly Othiambo (36), mpwa wa marehemu na mchimbaji wa madini, mkazi wa Buswelu – Ilemela, Erick Francis Olang (37), mfanyabiashara wa Kishiri – Nyamagana,
Abdul Nassir Dinisha (29), mfanyabiashara wa Nyamhongoro–Taiwan – Ilemela pamoja na Kulolwa Mbusu Muksen (46), mganga wa kienyeji wa Igoma – Nyamagana.
Ameeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alitekwa nyumbani kwake Katoro Geita, na kuingizwa kwenye gari aina ya Subaru Forester lenye namba T.927 DKW, kisha kusafirishwa hadi Mwanza kupitia barabara ya kuelekea Kayenze. Watuhumiwa hao walimnyonga hadi kufa na baadaye kutupa mwili wake ziwani kwa nia ya kuficha ushahidi.
Aidha, alieleza kuwa baada ya kufanya mauaji hayo, watuhumiwa walikimbilia kwa mganga wa kienyeji aitwaye Kulolwa Mbusu Muksen (46), kwa ajili ya kuoshwa dawa ili wasikamatwe na vyombo vya dola.
Kamanda alibainisha kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa ardhi unaohusiana na machimbo ya dhahabu yaliyopo Lwamgasa, mkoani Geita.
Alisisitiza kuwa watuhumiwa wote wameshikiliwa na watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika, huku akitoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya uhalifu na mauaji.
“Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha kila mtuhumiwa wa uhalifu anakamatwa na kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria alisema,kamanda Mtafungwa".
0 Comments