Taarifa kutoka vyanzo vya karibu na klabu hiyo zinasema kuwa kocha mkuu Mikel Arteta pamoja na uongozi wa juu wa Arsenal wameonesha nia ya kuimarisha safu ya ushambuliaji kwa kumsajili Gyökeres, ambaye kwa sasa ana kiwango bora na rekodi ya mabao inayovutia barani Ulaya.
Gabriel Jesus, ambaye alijiunga na Arsenal akitokea Manchester City mwaka 2022, amekuwa akikumbwa na majeraha ya mara kwa mara na kushindwa kuonyesha makali yake ya awali, jambo ambalo limechangia kupungua kwa nafasi yake katika kikosi cha kwanza.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, Arsenal ipo tayari kusikiliza ofa kutoka kwa vilabu vingine kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji huyo raia wa Brazil, ikiwa mpango wa kumsajili Gyökeres utakamilika.
Viktor Gyökeres, raia wa Sweden mwenye asili ya Hungary, aliweka rekodi ya kuvutia msimu uliopita akiwa na Sporting CP kwa kufunga mabao zaidi ya 40 katika mashindano yote, na amekuwa akihusishwa na vilabu mbalimbali vikubwa barani Ulaya, ikiwa ni pamoja na Chelsea na PSG.
Mashabiki wa Arsenal wanaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya usajili huo, huku matarajio yakiwa ni kuona timu yao ikipata mshambuliaji mwenye uwezo wa kubeba jukumu la kufunga mabao muhimu katika mbio za ubingwa.
0 Comments