Header Ads Widget

JE, TANZANIA IMEILENGA KENYA KUZUIA WAFANYABIASHARA WADOGO?

Katika kile kinachoonekana kama mwendelezo wa sera za kulinda uchumi wa ndani, Serikali ya Tanzania imetangaza rasmi marufuku dhidi ya shughuli 15 za kibiashara kwa raia wa kigeni.

Amri hii imezua hisia kali ndani na nje ya mipaka ya taifa hilo hasa kwenye mitandao ya kijamii, huku maswali mengi yakiibuka kuhusu malengo yake halisi. Ingawa waraka wa serikali haukutaja nchi yoyote, mjadala mkubwa umezuka nchini Kenya, ambako hisia za "kulengwa" na hatua hiyo zimeibuka.

Kwa upande wa Tanzania, serikali inasema hatua hiyo imelenga kulinda fursa za ajira, kipato na uwekezaji kwa wananchi wake hasa wale wanaojihusisha na biashara ndogondogo.

Lakini kwa upande mwingine, baadhi ya wanasiasa na wadau wa biashara wa Kenya wanasema wazi kuwa wameguswa moja kwa moja, wakiona huu kama mwendelezo wa kile wanachokiita "mtazamo wa kisiasa usio rafiki" kutoka kwa jirani yao wa kusini.

Kwa nini Serikali ya Tanzania imekuja na uamuzi huu?

Soko la Kariakoo

Kwa muda mrefu, wafanyabiashara wa kitanzania wamekuwa wakitoa malalamiko kuhusu kuongezeka kwa raia wa kigeni, hususan kutoka China, Kenya na India, wanaoingia kwenye biashara ndogondogo ambazo awali zilikuwa zikifanywa na Watanzania wenyewe.

Katika masoko kama Kariakoo, Mbagala na Karume, kumekuwa na ongezeko kubwa la maduka yanayoendeshwa na wageni, hasa Wachina, wanaouza bidhaa moja kwa moja kwa wateja kwa bei ya chini. Hali hiyo imewasukuma wazawa wengi kufunga biashara au kufanya kazi kwa hasara.

Mwaka jana, wafanyabiashara wa Kariakoo waligoma wakishinikiza serikali kushughulikia changamoto mbili kuu: moja ikiwa ni kodi kubwa wanazotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na ya pili ikiwa ni ongezeko la wafanyabiashara wa kigeni waliovamia sekta ya rejareja na biashara za mtaani.

Malalamiko haya yamekuwa yakijirudia katika maeneo mengi nchini, ambapo wageni wanadaiwa kuanzisha biashara bila kufuata taratibu, kuendesha shughuli zao kama familia bila kutoa ajira kwa wazawa, na kuuza kwa bei kandamizi ambayo inaleta ushindani usio wa haki.

Katika kukabiliana na hali hiyo, serikali iliunda kamati ya watu 15 kuchunguza mazingira ya wafanyabiashara wa kigeni na hasa athari zao kwa wafanyabiashara wa ndani katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam. Ripoti ya kamati hiyo, na vikao mbalimbali kati ya wafanyabiashara na Serikali, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, ndiyo msingi wa uamuzi huu wa sasa.

Biashara zilizopigwa marufuku kwa raia wa kigeni

Amri mpya inayojulikana kama Amri ya Leseni za Biashara (Marufuku ya Shughuli za Biashara kwa Wasio Raia), 2025, inabainisha wazi aina za biashara ambazo kuanzia sasa hazitafanywa tena na raia wa kigeni.

Kati ya shughuli hizo ni uuzaji wa bidhaa kwa rejareja, huduma za saluni, uhamishaji wa fedha kwa njia ya simu, na uanzishaji au uendeshaji wa vituo vya redio na televisheni.

Aidha, huduma za uongozaji watalii, uendeshaji wa mashine za kamari nje ya kasino rasmi, na kumiliki viwanda vidogo pia zimewekwa kwenye orodha hiyo.

Shughuli nyingine zilizozuiwa ni biashara ya uwakala wa fedha, udalali katika sekta ya ardhi na biashara, matengenezo ya simu na vifaa vya kielektroniki, huduma za usafi wa majumbani na maofisini, huduma za forodha na usafirishaji, pamoja na uchimbaji mdogo wa madini. Pia, wageni hawataruhusiwa kununua mazao moja kwa moja kutoka shambani.

Kwa mujibu wa amri hiyo, mamlaka zote za utoaji wa leseni nchini zimetakiwa kusitisha mara moja utoaji au upyaishaji wa leseni kwa wageni katika maeneo hayo. Wale ambao tayari walikuwa na leseni halali, wameruhusiwa kuendelea hadi leseni zao zitakapomalizika muda wake.

Adhabu kwa watakaokiuka ni kali: faini ya hadi shilingi milioni 10, kufutiwa visa na vibali vya ukaazi, au kifungo cha hadi miezi sita. Kwa Watanzania watakaobainika kuwasaidia wageni kuendesha biashara hizi kwa mgongo wa mbele, adhabu ni faini ya hadi milioni tano au kifungo cha miezi mitatu.

Kwa upande wa wafanyabiashara wa watanzania, wamefarijika kwa hatua hii. Mfaume Fadhili, Makamu Mwenyekiti Jumuia ya wafanyabiashara Kariakoo anasema: "Sisi tumepokea vizuri, tunaishukuru serikali na kuipongeza, kabla ya hapo kulikuwa na vikao vingi na serikali na baadaye serikali iligundua kwamba zipo biashara zinazofaa kufanywa na wazawa, zimeingiliwa na wageni kwa kiwango kikubwa".

Nini mtazamo wa wakenya ?

Seneta Joe Nyutu wa Kenya

Tangazo hili limepokewa kwa hisia tofauti nchini Kenya, ambapo maelfu ya raia wake wamewekeza au wanafanya kazi katika sekta zilizolengwa na amri hiyo. Wapo wanaounga mkono na wapo wanaoona kama ni hatua isiyostahili. Viongozi wa kisiasa na wadau wa biashara nchini humo wamelalamikia uamuzi huo wakisema ni wa kulenga moja kwa moja maslahi ya Wakenya walioko Tanzania.

Mmoja wa waliotoa kauli ya moja kwa moja kupitia runinga ya TV47 ni Seneta Joe Nyutu, ambaye alisema: "Marufuku hii, ingawa inawagusa wageni wote, inaelekezwa kwa Wakenya. Lakini hatupaswi kulipiza kisasi kwa sababu makosa mawili hayaleti haki." Kauli yake inaonesha hisia ya maumivu lakini pia wito wa kuhimiza uvumilivu na kutafuta njia ya mazungumzo ya kidiplomasia.

Kwa upande mwingine, Seneta wa zamani Ngunjiri Wambugu alichukua msimamo wa kuelewa hatua ya Tanzania, akisema: "Kwa mtazamo wa Kenya, tunahisi Tanzania wamekuwa haitendi haki'. Lakini ukiwa Mtanzania, unashindana kwenye biashara ndogo na wageni nafikiri wanajaribu kulinda watu wao."

Katika tasnia ya utalii, Victor Shitakha, Mwenyekiti wa Kenya Coast Tourism Association, alielezea masikitiko yake kwa uamuzi huo kwa kusema: "Ingawa naelewa lengo ni kulinda wananchi wake, lakini nimesikitika nchi kuchukua uamuzi wa aina hii. Nasikitika kwa uamuzi huu ambao unasababisha nchi zetu kutengana."

Msimamo mwingine umetolewa na Sam Ikwaye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kenya taasisi ya wahudumu wa hotel na wapishi, ambaye alionya kuwa kujilinda ni haki, lakini lazima pawe na mipaka. Alisema: "Ni jukumu la kila nchi kulinda wananchi wake na ajira zao, lakini lazima wazingatie kuwa hakuna nchi inayoweza kusimama peke yake. Ushirikiano wa kikanda ni nguzo muhimu kwa ustawi wa Afrika Mashariki."

Kuhusu la kulengwa wafanyabiashara fulani, Makamu Mwenyekiti wa wafanyabiashara Mfaume anasema; 'Hakuna wanaolengwa zaidi, isipokuwa wote wanaofanya biashara, kwa kulinda maslahi ya pande zote, sio biashara zote zimekatazwa ni biashara 15 pekee, zipo biashara ambazo wageni wanaendelea kufanya", anasema Mfaume na kuongeza faida ya hatua hii kwao na Tanzania: "Ikiwa biashara anafanya mfanyabiashara fulani haikingiliwi na mgeni maana yake mtaji (wa mtanzania) utakuwa, ataajiri na serikali itapata kodi".

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI