Na Fatma Ally Matukio na Habari App
Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya (DCEA) imesema imebaini mbinu mpya inayotumiwa na wahalifu wa dawa za kulevya kwa kutumia maiti za binaadam kusafirishia dawa za kulevya kutoka nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo amesema wahalifu hao hutumia fuvu la kichwa la maiti ya binadam kulifungua na kutoa ubongo na kujaza dawa za kulevya pamoja na kuwapasua kifua na tumbo kuweka dawa za kulevya.
"Wahalifu wa dawa za kulevya wana kila mbinu lakini nataka kuwahakikishia kuwa na sisi tupo macho kila watakapokanyaga na sisi tupo, wanatumia maiti zinazosafirishwa kutoka nje ya nchi kuja Tanzania kuwabebesha dawa za kulevya, wanawatoa mapafu na chango zote zilizotumboni ili kuweka dawa za kulevya"amesema Kamishna Lyimo.
Aidha, amewaonya ndugu wanaosafirisha maiti zinazofariki nje ya nchi kwenda Tanzania, kuhakikisha wanasimamia mwanzo hadi mwisho wa usafirishaji huo kwani endapo maiti itabainika kubebeshwa dawa za kulevya lazima ndugu watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Sambamba na hilo DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanya oparesheni katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania na kukamata dawa za kulevya jumla ya kilogram 37,197.142.
Kamishna Lyimo amesema kuwa, dawa hizo zimejumuisha kilogram 11,031.42 za dawa za kulevya aina ya Mitragyna speciosa.
Ametaja dawa nyengine ni bangi kilo 24,873.56, mirungi kilo 1,274.47, skanka kilo13.42 , heroin kilo 2.21, na methamphetamine gram 1.42 pia ukamataji huo umehusisha dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya ketamine kilo1.92.
Aidha, katika oparesheni iliyofanyika bandari kavu eneo la Temeke jijini Dar es Salaam kilo 11,031.42 za dawa za kulevya aina ya Mitragyna speciosa zilizoingwa nchini kutoka nchini Sri Lanka zilikamatwa zikiwa kwenye vifungashio vyenye chapa inayoonesha kuwa ndani yake kuna mbolea .
Hata hivyo, oparesheni iliyofanyika Posta Dar es Salaam wamekamata watuhumiwa sita wakiwemo raia wawili wa china wanaofahamika kwa majina ya Chein Bai na Qixian Xin walikamatwa wakisarisha dawa za kulevya aina ya methamphetamine gram 1.42 dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya frunitrazepam vidonge 1000 na ketamine zenye uzito wa kilo 1.92.
Katika hatua nyengine eneo la Sinza walikamatwa watu wawili wamiliki wa kiwanda bubu kinachotengeneza biskuti zinazochanganywa na bangi kisha kuzisambaza katika mikoa ya Dar, Mwanza, Lindi na Mtwara, wakati huo huo mkoani Lindi alikamatwa mfanyabiashara wa madini akisambaza biscuit hizo.
0 Comments