WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga, amesema matarajio ya serikali kupitia maonesho ya utalii na uwekezaji ni kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua kwa kasi na kufikia hadhi ya maonesho bora na makubwa zaidi barani Afrika, hususan katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kauli hiyo aliitoa wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya kufanyika kwa maonesho hayo ya pili Juni 20 mwaka huu katika viwanja vya Maonesho Nyamanzi.
Alisema lengo kuu ni kuyafanya maonesho hayo kuwa jukwaa muhimu la kukuza utalii, kuvutia wawekezaji wapya na kuimarisha uhusiano baina ya wadau wa sekta ya utalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Aidha alisema maonesho mwaka huu yatainesha vivutio vya utalii Unguja na Pemba na kuhakikisha yanafikia viwango kama wanavyoshudia kwa wenzao kama kill fear, ITB, WTM na wengine.
Waziri Soraga, alisema lengo jengine ni kuitangaza hadhi ya Zanzibar kwani serikali inachukua jitihada mbalimbali kutangaza visiwa na kutoa ujumbe wa nini hasa Zanzibar inasimamia ili iweze kufanya hivyo kwa ufanisi ni lazima iwe na matukio kama hayo ambayo yanawaleta pamoja wadau wa ndani na nje ya nchi.
“Tunataka haya maonesho yawe ya kipekee barani Afrika. Kwa kupitia ushiriki wa taasisi za kimataifa, watoa huduma za utalii, wawekezaji, na wadau mbalimbali, tunaamini Zanzibar itazidi kujitangaza duniani kama kivutio kikuu cha utalii na uwekezaji,” alisema Waziri Soraga.
Aliahidi kuwa mwaka huu watashirika wanunuzi na waoneshaji wa bidhaa wa ndani pekee lakini mwakani watakaporejea kufanya maonesho hayo kuwa ya kimataifa kwa kutoa mualiko kwa watu hao nje ya Afrika Mashariki na sehemu nyengjne duniani.
"Hii ni hatua yetu ya pili kuitangaza na kuikuza Zanzibar kupitia maonesho haya na kuipa baina ya kimataifa kwani tukio hili limelenga kuleta watu pamoja na kupeana fursa ikiwemo kubadilishana biashara n ahata uzoefu," alisema.
Hivyo, alisema ni imani yake kuwa wakienda huko watazidi kutanua wigo lakini kuleta taswira ya kimataifa kwani maonesho hayo hayatafanyika Zanzibar pekee bali duniani kote.
Alisema anaamini muelekeo walionao na mageuzi makubwa yanayoonekana kipindi kifupi watakuwa na uwezo wa kufikia huko kwani yapo mambo mazuri wanayotaka kuyaonesha na anaamini maonesho hayo yatatoa fursa pana zaidi ya kutangaza vivutio vilivyopo na kutoa fursa kwa wadau kuvutia uwekezaji katika visiwa vya Zanzibar.
Sambamba na hayo, alisema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha mazingira ya uwekezaji na biashara katika sekta ya utalii yanaboreshwa kwa manufaa ya taifa na wananchi kwa ujumla.
Maonesho hayo yanatarajiwa kuleta msukumo mpya katika kuongeza idadi ya watalii, kuimarisha mapato ya taifa na kukuza ajira kwa vijana wa Zanzibar kupitia shughuli za utalii na huduma zinazohusiana.
Hivyo aliwaomba wadau wa sekta za biashara na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia kazi nzuri ya kutangaza utalii na kuonesha vituvito vyake katika visiwa vya Unguja na Pemba.
0 Comments