Na COSTANTINE MATHIAS, Nyangh'wale.
WAKULIMA wa Pamba wilaya ya Nyangh'wale Mkoani Geita, wametakiwa kuzingatia kanuni za kilimo cha Pamba ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea ili waweze kuongeza tija ya uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.
Hatua hiyo imekuja baada ya wakulima hao kuongeza uzalishaji kutoka kilo 300 kwa ekari moja na kufikia kilo 1000 hali inayoelezwa kupiga hatua kwenye uzalishaji na Maendeleo ya sekta ya Pamba.
Hayo yamebainishwa jana na Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo, Gudala Kija wakati akikagua Ubora wa Pamba kwenye vituo vya kununulia Pamba vya Bukwimba Amcos pamoja na kuongea na Wakulima ambapo alisisitiza pia uvunaji salama ili kuendelea kulinda Ubora wa Pamba.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika sekta ya kilimo kwa kutoa ruzuku ya Pembejeo ikiwemo mbegu na madawa ili kuhakikisha mkulima wa Pamba anapata huduma za Ugani Kwa wakati.
"Lengo la serikali ni kuzalisha kwa tija kutoka kilo 200 mpaka kilo 1000 kwa ekari moja, kuna wakulima wameanza kufikia lengo hilo...tunafanya jitihada pamoja na serikali kuleta ruzuku ya mbolea na mbegu, tunawashauri wakulima wenye Mifugo watumie mbolea ya samadi ili kuongea tija ya uzalishaji" amesema Gudala.
Akizungumza hali ya uzalishaji kwa ujumla, Gudala amesema kuwa katika misimu mitatu iliyopita, 2021/2022 Kilo 2,174,200 na 2022/2023 uzalishaji ni Kilo 3,166,230 na misimu 2023/2024 ni Kilo 838,790.
Kawawa Luduko, mkulima kiijii Cha Bukwimba amewasisitiza wakulima kufuata kanuni za kilimo cha Pamba ikiwemo kuvuna kwa wakati ili Pamba isipoteze Ubora.
Amesema kutokana na Mafunzo wanayopata, wakulima hao (akiwemo yeye) wameongeza uzalishaji kutoka kilo 300 mpaka 1000 kwa ekari moja jambo ambalo limeonyesha Mafanikio na kujikwamua kiuchumi.
Paulo John, mkulima Kijiji Cha Bukwimba amesema zao la pamba limewatia kwenye umaskini huku akiiomba serikali kuongeza ili waongeze uzalishaji.
'Tulime Pamba Kwa kufuata kanuni ili kupata uzalishaji Mkubwa, tupanda kwa wakati, tuvuna kwa wakati, pamba ikichelewa kuvunwa itapunguza Ubora...wanaoendelea kuchafua Pamba wakamatwe Kwa Mujibu wa Sheria, tusibebe Pamba kwenye sandarusi sababu nyuzi zinaharibu mashine, na kushusha Ubora wa Pamba" amesema Thomas Kabumutime, mkulima Kijiji Cha Bukwimba.
Mwisho.
0 Comments