NA ALI RASHID.
“Sheria ni msingi wa haki amani na maendeleo kwa kila nchi “Hayo si maneno yangu bali yalikuwa ni maneno ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizindua toleo jipya la juzuu za sheria mwezi Aprili ,2025 jijini Dar es salaam.
Anasema, bila ya sheria kuwa wazi uhakika wa ulinzi wa haki za raia unatoweka au unakuwa hauna uhakika na kusababisha uvunyifu wa amani.
Wandishi wa Habari Zanzibar wamekuwa wakidai sheria nzuri na rafiki ya habari bila ya mafanikio yoyote.Kutokana na kutumia sheria ya zamaani na iliyopitwa na wakati iliyotungwa tokea miaka ya 1988 ambayo kwa sasa ni kikwazo kwa wandishi wa habari.
Akizungumzia kuhusu sheria hiyo, mwandishi nguli wa habari visiwani Zanzibar, Salma Lusangi anasema ni muhimu kwa sasa sheria hiyo ibadilishwe ili iendane na wakati na kukidhi matakwa ya wakati husika.
“Kwa kipindi kirefu tumekuwa tukifanya uchechemuzi wa sheria mbili kuu yaani sheria ya Wakala wa Habari Magazeti na Vitabu ya mwaka (1988) na sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar (1997) ambazo waathirika wakubwa ni wandishi wa habari na jamii kwa ujumla” anasema Salma na kuongeza kuwa.
“Sheria za Habari zilipotungwa kulikuwa hakuna mitandao ya kijamii ila sasa tuna mitandao ya kijamii hivyo ni lazima twende na wakati, sheria iifanyiwe marekebisho ili iwe rafiki na ilete tija”.
Salim Said ni mhariri na Mjumbe wa Jukwaa la Wahiriri Tanzania TEF anasema anaamini kwamba nia ya kupatikana sheria mpya ya habari haipo kwa Serikali ya Zanzibar, kwani haitaki kuifanyia kazi suala la marekebisho ya sheria za habari na badala yake imekuwa ikifanya udanganyifu kwa kutoa ahadi za uongo.
“Tokea suala hili lizungumzwe na sisi wadau wa habari, tumekuwa tukipewa ahadi tofauti, mfano tupo njiani, tupo mbioni hizo hazina mwanzo wala mwisho, hata Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi alipoingia madarakani tulikutana nae, alituahidi hivyo na mpaka sasa hakuna kilichofanyika” anasema Salim.
Salim hakuishia hapo anaona kuwa Waziri wa Wizara hiyo Tabia Maulid Mwita imekuwa tabia yake , kila anapoulizwa kwa takribani mara tatu 3 ameahidi mswada huo utasomwa katika Baraza la Wakilishi ahadi ambayo hadi sasa haijatimia.
“Katika miaka 20 hii tunayopigania uhuru wa habari, tunashuhudia Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepokea na kuzirekebisha au kutunga sheria zaidi ya 10 lakini wanaifumbia macho sheria ya habari”.
Anawasihi viongozi kuiga mifano ya nchi jirani na wanapaswa kujiuliza kwanini nchi kama Uganda, Rwanda na Tanzania bara wamefanya marekebisho ya sheria na kuweka mazingira mazuri ya waandishi wa habari kupaza sauti zao na kutoa maoni ya wananchi.
Kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025, wandishi wa habari wanabanwa kufanya kazi zao kwa uwazi na wanapojaribu kuhoji kuhusiana na kitu fulani wanaitwa wachochezi.
Mwanaharakati na mtetezi wa maswala ya habari Zanzibar Juma Khamis Juma, anasema sheria ya habari ni muhimu katika kuimarisha uhuru wa kujieleza na kutoa maoni katika nchi yoyote duniani.
“Zanzibar ni sehemu ya nchi hizo, ingawa sheria iliyopo ni ya muda mrefu ambayo imetungwa tokea mwaka 1988, miaka mitatu ijayo itatimiza miaka 40, hivyo bila shaka kuna haja ya kuwa na sheria mpya ya habari”.
Juma anaogeza kuwa, sheria ya sasa ya habari ina changamoto ambazo wadau wanaamini zinawakwaza katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo mamlaka makubwa aliyopewa askari polisi kuingia katika chombo cha habari bila ya idhini au kwa idhini ya mahkama.
“Sheria pekee haiwezi kusaidia kuboresha mazingira ya kazi, lakini uwepo wa sheria na utashi wa kuitekeleza ndio utaleta mabadiliko yenyewe”.
Suala la haki za kibinaadam linalenga pia uwepo wa sheria zinazoangalia mustakbali wa uhuru wa kupata, kutafuta na kupokea taarifa au habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msaada wa Kisheria Zanzibar (ZALHO) Harusi Miraji Mpatani anasema suala la uhuru wa habari ni suala la haki ambayo imeelezwa katika kifungu cha 18 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo inasema kila raia ana haki ya kutoa na kupokea taarifa.
“Tunahitaji sheria ambazo zitaamini kuwa suala la habari ni suala la haki, ambayo inatakiwa kutolewa bila ya makando kando yoyote ambayo unapewa kwa mkono wa kushoto na unanyang’anywa kwa mkono wa kulia” anasema Harusi kwa msisitizo huku akiongeza kuwa kuna athari kubwa kwa jamii kama hakuna sheria nzuri za habari kwani kutapelekea kuenea kwa habari zisizo sahihi.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA-Z wamekuwa katika harakati za mageuzi kwenye suala la uhuru wa habari na kupatikana kwa sheria nzuri zitakazolinda maslahi na usalama wao.
Afisa mradi wa masuala ya utetezi na uchechemuzi kutoka TAMWA-Z Zaina Abdallah Mzee anasema kuwa wanachukuwa jitihada mbalimbali za kuzisemea sheria zote zinazohusu habari ambazo haziko huru na rafiki kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari ambazo ni sheria ya Wakala wa Habari Vitabu na Magazeti ya mwaka 1988, Sheria ya Tume ya Utangazaji, Sheria ya Uchaguzi na nyenginezo ambapo sheria zote hizi zinawagusa waandishi wa habari na vyombo vya habari na badala yake kupendekeza kuwekwa sheria moja tu ambayo ni rafiki kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari katika kazi zao.
“Tumekuwa tukipaza sauti zetu kwa muda mrefu sasa kupatikana sheria mpya ya habari Zanzibar kuzisemea sheria ambazo zina mapungufu kwa waandishi wa habari na badala yake kupendekeza sheria moja tu ambayo ni rafiki kwa waandishi wa habari”.
Zaina anaelezea mashirikiano yao baina ya Kamati ya Wataalam wa Masuala ya Habari Zanzibar ZAMECO na serikali ikiwa ni pamoja na kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi akiwemo Rais na Waziri wa Habari ,Tume ya kurekebisha sheria ,Idara ya habari maelezo na wajumbe wa baraza la wawakilishi ambapo wote hawa wamekiri kuwepo kwa mapungufu katika sheria ya habari iliyopo.
“Mashirikiano ni mazuri baina yetu na serikali kwani tumepata kufanya mazungumzo na viongozi mbali mbali wa nchi na wao wamekiri kuwepo kwa mapungufu katika sheria ya habari iliyopo na kuwahidi kufanyia marekebisho”.
Abdallah Mfaume ni mjumbe wa Kamati ya Wataalam wa Masuala ya Habari Zanzibar ZAMECO anasema kuna umuhimu mkubwa wa kuharakishwa kwa sheria mpya ya habari ili iwasaidie waandishi wa habari hasa katika kutekeleza majukumu yao.
“Waandishi wa habari wanahitaji utulivu, usalama na ulinzi ili jamii inufaike kupitia fani hiyo ambayo ndiyo yenye jukumu la kuhabarisha jamii”.
Baraza la Habari Tanzania MCT lilikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kunawepo kwa mabadiliko ya Sheria za Habari Tanzania bara wakifanya shughuli zao hapa Zanzibar wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sheria mpya na rafiki kwa wana habari.
Ziada Kilobo ni Msimamizi wa Ofisi ya Baraza la Habari Tanzania upande wa Zanzibar anasema kuwa suala la sheria nzuri za habari ni suala la kupewa kipaombele hasa kwa nyakati hizi ambazo tunaelekea kwenye uchaguzi.
“Kukiwa na sheria nzuri wanahabari wanaweza kuwasaidia wakafanya kazi zao kwa weledi na kuna umuhimu wa kuwa na sheria mpya na zenye kulinda maslahi ya waandishi na hata jamii”
Ziada ameongeza kuwa kwa upande wa serikali ni vyema kuona suala hili kuwa linahusua maisha ya jamii zaidi.
“Serikali ione suala hili kuwa ni muhimu kwa nchi na kwa jamii maana uhuru wa Habari ni suala linalotoa nafasi kwa waandishi kuzisemea changamoto na mafanikio yaliyopo kwenye jamii yao”.
0 Comments