Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Mashariki ya Kati imegeuka kuwa kitovu cha mivutano ya kijeshi isiyokuwa na mwisho tangu vita vya Iraq au vita vya Yom Kippur. Kati ya nchi zote zilizoathirika, Israel imesimama kati kati ya joto la vita, ikikabiliana na mashambulizi kutoka pande tofauti, huku maadui wa jadi wakirudi kwa nguvu mpya.
Kuhusu mzozo wa sasa ni mvutano kati ya Israel na Iran, mvutano uliofikia hatua ya hatari mnamo Juni 2025 baada ya mashambulizi ya wazi kati ya nchi hizo mbili, hali ambayo haikuwahi kushuhudiwa kwa kiwango hiki.
Iran, kwa miongo kadhaa, imekuwa ikiendesha vita vya kivuli dhidi ya Israel kwa kutumia makundi ya wapiganaji kama Hamas, Hezbollah, Houthi na makundi ya wanamgambo wa Kishia katika Iraq na Syria. Israel, kwa upande wake, imekuwa ikitumia njia za kijasusi na mashambulizi ya angani kukata ushawishi wa Iran.
Hata hivyo, kwa sasa, hali imebadilika. Haya si tena mashambulizi ya siri au ya kiwakala; ni vita vya moja kwa moja vinavyohusisha mashambulizi ya makombora, ndege za kivita, vifo vya raia, na taharuki ya kimataifa.
Makala hii inachambua vita vitano vikuu ambavyo Israel inapigana navyo kwa sasa, ikianzia na lile linaloonekana kama kiini cha mzozo wote, vita dhidi ya Iran.
1. Vita dhidi ya Iran
Vita kati ya Israel na Iran vilianza rasmi mnamo Juni 12, 2025, wakati Israel ilipoanzisha mashambulizi ya anga yaliyopewa jina la "Operesheni Simba" dhidi ya vituo vya nyuklia na kijeshi vya Iran, hasa karibu na Tehran, Isfahan na Natanz. Hili lilifuatia miezi kadhaa ya kuongezeka kwa mivutano, baada ya Iran kudai Israel ilihusika na mauaji ya jemedari wake wa juu wa kijeshi nchini Syria.
Iran ilijibu mapigo mashambulizi ya makombora ya masafa marefu dhidi ya miji ya Tel Aviv, Ashkelon, na maeneo ya kijeshi ya Israel. Hii ilikuwa mara ya kwanza tangu Mapinduzi ya kiislamu ya 1979 ambapo Iran na Israel wameingia kwenye vita vya moja kwa moja.
Vita hivi vinashirikisha pia nguvu zingine za kikanda. Marekani imekuwa ikiunga mkono Israel kwa kutoa msaada wa ujasusi na vifaa, ingawa haijajiingiza moja kwa moja kijeshi. Urusi na China zimekuwa kimya, lakini zimesisitiza umuhimu wa mazungumzo.
Nchi za Kiarabu kama Saudi Arabia na Misri zimeelezea hofu yao kuhusu uwezekano wa vita ya kikanda. Rais wa Marekani, Donald Trump anasema kuna hatua zaidi ya kuchukuliwa zaidi ya kusitisha vita.
Athari za vita ni kubwa. Kufikia katikati ya Juni 2025, zaidi ya watu 400 wamekufa Iran, wengi wao katika mashambulizi ya anga, huku zaidi ya Waisraeli 70 wakiuawa katika mashambulizi ya makombora ya Iran. Uchumi wa Iran umetikiswa vibaya, na Israel imeweka majeshi yake katika hali ya tahadhari ya juu.
Kwa sasa, hali ni tete sana, mashambulizi yanaendelea, na hakuna upande unaoonyesha nia ya kusitisha vita.
2. Vita dhidi ya Hamas
Vita vya Israel dhidi ya Hamas vilizuka upya kwa nguvu mnamo Oktoba 7, 2023, baada ya shambulio la ghafla na la kushangaza lililofanywa na wanamgambo wa Hamas dhidi ya maeneo ya kusini mwa Israel, likisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200. Shambulio hilo liliibua hasira kubwa kutoka kwa Israel, ambayo ilizindua operesheni ya kijeshi ya muda mrefu katika Ukanda wa Gaza.
Israel inapigana pia na makundi mengine ya wanamgambo wa Kipalestina, ukiacha Hamas na Islamic Jihad, yanayojikita katika Ukanda wa Gaza.
Katika kipindi cha miezi 18 iliyofuata, Israel ilifanya mashambulizi ya angani, ardhini na baharini dhidi ya Gaza, ikilenga miundombinu ya Hamas, vichochoro vya chini ya ardhi, maghala ya silaha na viongozi waandamizi wa kundi hilo. Hamas, kwa upande wake, ilijibu kwa kurusha roketi zaidi ya elfu kumi kuelekea Israel.
Nchi mbalimbali zimehusika moja kwa moja au kwa njia ya upatanishi. Qatar na Misri zimekuwa wakuu wa majadiliano ya upatanisho. Iran imekuwa mtoa msaada mkuu wa silaha kwa Hamas, huku nchi za Magharibi zikiunga mkono haki ya Israel kujilinda, japo kwa masharti ya kutoathiri raia.
Kufikia Juni 2025, zaidi ya Wapalestina 35,000 wamekufa, huku zaidi ya Waisraeli 1,500 wakiuawa tangu kuanza kwa vita. Vita bado vinaendelea, ingawa kwa sasa ni ya kiwango cha chini ambapo Israel inaendelea na mashambulizi ya kulenga wahamas ndani ya Gaza.
3. Vita dhidi ya Hezbollah
Hezbollah ni kundi la kisiasa na kijeshi la kishia lenye makao yake Lebanon, linaloungwa mkono na Iran. Tangu 2006, Israel na Hezbollah wamekuwa na mivutano ya mara kwa mara, lakini vita vya wazi vilizuka upya baada ya kuanza kwa operesheni ya Gaza mnamo Oktoba 2023.
Hezbollah ilianza kurusha makombora na kutuma wapiganaji wake kuvamia maeneo ya kaskazini mwa Israel kama ishara ya mshikamano na Gaza. Israel ilijibu kwa mashambulizi ya angani dhidi ya ngome za Hezbollah kusini mwa Lebanon na katika mpaka wa Syria.
Mashambulizi haya yamesababisha vifo vya zaidi ya raia 500 nchini Lebanon, huku zaidi ya wanajeshi na raia 200 wakiuawa Israel. Mamilioni ya watu wameyahama makazi yao pande zote mbili.
Ufaransa na Marekani zimejaribu kupatanisha, lakini Iran imeapa kuendelea kuunga mkono Hezbollah. Vita hivi bado vinaendelea kwa kiwango cha wastani, lakini kuna hatari kubwa ya kuongezeka kuwa vita kamili na kubwa.
4. Vita dhidi ya Houthi
Kundi la Houthi, linalotawala sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen, limekuwa likishambulia Israel kwa makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani (drones) tangu mwishoni mwa 2023, likidai kuwa linaitetea Palestina dhidi ya "udhalimu wa Kizayuni".
Mashambulizi haya yamekuwa yakipitia bahari ya Shamu, na baadhi yamelenga miji ya kusini mwa Israel pamoja na meli za kibiashara zinazohusiana na Israel. Kwa kujibu, Israel imefanya mashambulizi ya angani dhidi ya vituo vya makombora vya Houthi nchini Yemen.
Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambao nao wamekuwa katika vita na Houthi kwa muda mrefu, wameunga mkono chinichini mashambulizi ya Israel, huku Iran ikiendelea kuwa mdhamini mkuu wa Houthi.
Athari za vita hivi mpaka sasa ni pamoja na kuvuruga biashara ya kimataifa kupitia Bahari ya Shamu, vifo vya raia kadhaa nchini Yemen, na kuongezeka kwa taharuki ya kijeshi katika pembe ya Afrika.
5. Vita dhidi ya makundi ya wanamgambo Iraq na Syria
Kwa muda mrefu, Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya siri dhidi ya wanamgambo wa kishia wanaoungwa mkono na Iran katika nchi za Syria na Iraq. Hata hivyo, tangu kuanza kwa vita vya Iran-Israel mnamo Juni 2025, mashambulizi haya yameongezeka na sasa yamepata sura ya wazi zaidi ya vita.
Makundi kama Harakat al-Nujaba, Kataib Hezbollah na Asaib Ahl al-Haq yameshambulia maeneo ya Israeli kupitia Syria au Iraq, huku yakitoa kauli za kuunga mkono Iran. Israel imejibu kwa kushambulia misafara ya silaha, maghala, na kambi za mafunzo za wanamgambo hao.
Hali ni tete, na mashambulizi haya mara nyingi huambatana na vifo vya viongozi wa ngazi za juu wa wanamgambo, na kuibua maandamano na machafuko katika maeneo ya Kisuni nchini Iraq.
Mataifa ya Magharibi yameendelea kuwa waangalizi wa karibu wa mgogoro huu, kwa hofu kuwa mapigano haya yanaweza kugeuka kuwa janga la kanda lote.
0 Comments