Na. Jacob Kasiri - Dar es Salaam.
Slogan ya “TANAPA nyumbani kwa Tuzo” imetamalaki leo June 02, 2025 wakati Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) walipopokea tuzo ya utoaji huduma bora kwa viwango vya kimataifa (European Award for Quality Choice Achievement 2025) Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ikitokea Stockholm Sweden. Tuzo hiyo iliyotolewa na Jumuiya ya Ulaya inayohusika na utafiti wa viwango vya huduma bora za kimataifa (European Society for Quality Research ESQR).
Tuzo hiyo inayolitambulisha shirika hilo kimataifa ilipokelewa leo jijini Dar es Salaam chini ya ujumbe wa TANAPA ulioongozwa na Kamishna wa Uhifadhi wa shirika hilo CPA (T) Musa Nassoro Kuji.
Wakati wa mapokezi hayo Kamishna Kuji alisema,”Ushindi wa tuzo hii kwa mara ya sita mfululizo sasa unatuongezea hamasa na ari kwa taasisi yetu inayosimamia Hifadhi za Taifa 21 ili tuendelee kutoa huduma bora kwa watalii sanjari na kukidhi matamanio yao ili kuendelea kuliheshimisha taifa la Tanzania Kimataifa.l
Aidha, Kamishna Kuji aliongeza, “Utoaji wa huduma bora ni tabia na utamaduni wetu tuliojijengea kama TANAPA, hivyo tuwahakikishie Watanzania na dunia kwa ujumla, tutaendelea kutoa huduma bora ili watalii hao wafurahie vivutio vyetu na waendelee kumiminika kuja Tanzania kwa ajili ya kuliongezea taifa mapato yatokanayo na utalii.”
Vile vile, Kamishna Kuji alisema kuwa anaitoa tuzo hiyo maalumu kwa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake binafsi za kuitangaza Tanzania na kuwa nchi inayoshika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio bora zaidi, hata hivyo Mhe. Rais amevitangaza kupitia filamu mbili zenye thamani kubwa "Tanzania: The Royal Tour na “Amazing Tanzania".
Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini alisema kuwa tuzo hii inatokana na juhudi kubwa kutoka Wizara ya Maliasili na utalii, TANAPA na wananchi kwa ujumla kwani ushirikiano wao ndio msingi wa mafanikio ya tuzo hii na tuzo nyingine ambazo shirika limeendelea kuzipata.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwell Meng’ataki, Mkuu wa Kanda ya Kusini aliyekuwa kwenye msafara wa TANAPA waliokuwa Sweden, alisema kuwa tuzo hiyo ni ishara ya mafanikio makubwa kati ya nchi 42 zilizoshiriki katika mchakato huo.
“Kupitia tuzo tumejifunza mengi ambayo yatakuwa msingi wa kuendelea kutoa huduma bora na za viwango vya juu ili tuendelee kushinda tuzo, kwani ushindi huu unaiongezea TANAPA na Tanzania kujulikana kimataifa hivyo kuwa hamasa kwa wageni wengi kuitembelea Tanzania”, aliongeza Kamishna Meing’ataki.
Tuzo hii ya ESQR 2025 ambayo TANAPA wameshinda usiku wa Mei 29, 2025 ni kutokana na kutoa huduma bora ambazo zimetambulika kimataifa na TANAPA imeendelea kuipata kwa mara ya sita mfululizo kuanzia mwaka 2020 hadi 2025.
0 Comments