Na Matukio Daima Media ,Iringa
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Abri Asas, amesema kuwa ni wajibu wake mkubwa kuhakikisha chama chake pamoja na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wanapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao, huku akianza harakati hizo kutoka nyumbani kwake, mkoa wa Iringa.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wana CCM waliojitokeza kwa wingi katika viwanja vya CCM mkoa wa Iringa kwa ajili ya kumpokea, Asas alieleza kuwa uteuzi wake kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ni heshima kubwa sio tu kwake binafsi, bali kwa wana CCM wote wa Iringa waliompa ridhaa kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho.
“Asanteni sana wana CCM kwa mapokezi haya makubwa nafasi hii niliyopewa siyo ndogo ni dhamana ya juu kabisa ndani ya chama chetu na ninapokea kwa unyenyekevu mkubwa nitahakikisha nainatendea haki nitaanza na mkoa wangu wa Iringa kuhakikisha tunaleta ushindi wa kishindo kwa Rais Dkt. Samia pamoja na wagombea wote wa CCM,” alisema Asas huku akishangiliwa na umati wa wana CCM waliokuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za hamasa.
Asas alisema kuwa nafasi hiyo ya mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa (CC) inamwezesha kushiriki moja kwa moja katika vikao vya juu vya maamuzi, ikiwemo mchakato wa kupitisha na kuchuja majina ya wagombea katika ngazi mbalimbali.
Hivyo aliahidi kutumia nafasi hiyo kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia maslahi ya chama na wanachama wake.
Aliongeza kuwa licha ya kupanda ngazi hiyo ya juu, ataendelea kuwa yule yule, mwanachama mtiifu na mchapakazi ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha siasa za maendeleo na mshikamano ndani ya chama.
Alisema kuwa ataendelea kushiriki moja kwa moja katika harakati za kutafuta ushindi, akisema atazunguka mtaa kwa mtaa, kata kwa kata, hadi mkoa kwa mkoa, kuhakikisha ushindi mkubwa kwa CCM unapatikana.
“Asitokee mtu akadhani kuwa nafasi hii itanibadilisha mimi nitabaki kuwa mwanachama yule yule wa kawaida Nitashuka kwa wananchi, nitazungumza nao, nitawaeleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu Dkt. Samia, na nitaomba kura kwa ajili yake na kwa ajili ya CCM,” alisema kwa msisitizo.
Katika tukio hilo la mapokezi, viongozi na wanachama mbalimbali walipata nafasi ya kutoa salamu na kumpongeza Salim Asas kwa kuteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu.
Wakili Sosten Mbedule kutoka Jimbo la Kalenga alisema kuwa hotuba ya Asas imeonesha kiwango kikubwa cha busara, unyenyekevu na uelewa wa siasa za chama hicho.
“Kwa nafasi hii aliyoipata, mtu mwingine angeweza kuanza kujiona mkubwa na kuwa mbali na wananchi lakini ndugu yetu Salim ameonesha namna alivyo na moyo wa kuitumikia CCM na kuwasikiliza wanachama. hii ni hatua kubwa ambayo inatufundisha kuwa uongozi si nafasi ya kujinufaisha bali ni huduma kwa umma,” alisema Mbedule.
Wakili Moses Ambwindwile kutoka Iringa Mjini pia alieleza kuwa Asas ni kiongozi mwenye dira, na maneno yake yamejaa maono ya mshikamano ndani ya chama.
Aliongeza kuwa iwapo viongozi wengi wa chama watakuwa na mtazamo kama wa Asas, basi CCM itaendelea kuwa chama madhubuti na chenye mvuto kwa wananchi.
Jasmine Ng’umbi, mjumbe wa kamati ya utekelezaji UVCCM Wilaya ya Mufindi, alisema kuwa vijana wa CCM wanajivunia kuwa na kiongozi kama Asas, ambaye si tu ni mzoefu bali pia ni kielelezo cha kiongozi anayejitoa kwa ajili ya maslahi ya wengi.
Alisema kuwa vijana wataendelea kumuunga mkono ili kuhakikisha malengo ya chama yanafikiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yassin, aliwashukuru wana CCM kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mapokezi ya Salim Asas.
Alisema kuwa ujio wa Asas kama mjumbe wa Kamati Kuu ni fursa kwa mkoa wa Iringa, kwani sasa wana sauti ya moja kwa moja katika vikao vya juu vya chama.
“Tunampongeza kwa kuteuliwa lakini pia tunamtakia kila la heri katika kutekeleza majukumu yake hii ni nafasi ya mkoa wetu kuhakikisha tunashiriki kikamilifu katika kuhakikisha Rais wetu Dkt. Samia, wabunge na madiwani wote kutoka CCM wanapata ushindi wa kishindo tuendelee kushikamana,” alisema Yassin.
Mapokezi hayo yalipambwa na vikundi mbalimbali vya burudani, ngoma za asili, gwaride la vijana wa UVCCM pamoja na maandamano ya wanachama kutoka kata mbalimbali za manispaa ya Iringa.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, uteuzi wa Salim Asas unaonesha imani kubwa ya chama kwa viongozi wanaotoka katika maeneo ya ndani ya nchi, na ni dalili ya jinsi CCM inavyojipanga kuwa na sura jumuishi katika safu ya juu ya uongozi wake.
0 Comments