Header Ads Widget

OFISI YA RAIS IKULU YATAKA WATUMISHI WANAOSHUGHULIKIA MALALAMIKO YA WANANCHI KUBADILIKA


 Na Matukio Daima App.

MOROGORO.OFISI ya Rais Ikulu imewataka watumishi wa taasisi za umma wanaoshughulikia sheria na malalamiko ya wananchi kuwajibika ipasavyo kutatua changamoto za wananchi Ili kuondoa ongezeko la malalamiko kufikishwa moja kwa moja kwa vingozi wa juu wa nchi akiwemo Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Katibu Mkuu kiongozi.

Aidha Serikali haitavumilia uzembe unaofanywa na baadhi ya watumishi wa umma kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo katika majukumu yao kwani malalamiko kufikishwa ngazi za juu kutokana na uzembe wao ni ukiukwaji wa sheria na ni utovu wa nidhamu ambao hauvumiliki.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu,Mululi Mahendeka, amesema hayo Mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo kwa baadhi ya watumishi wa taasisi za umma wanaoshughulikia sheria na malalamiko ya wananchi.

Akawataka wanaofanya hivyo kuacha mara moja na kwamba masuala yaliyo ndani ya uwezo wao hawana budi kuyamaliza wenyewe kwa haraka na kwa usahihi.

"Pale unapoona huna uhakika na kile unachopaswa kufanya juu ya jambo la mbele yako, usilisukumie ngazi nyingine, au kumuacha mwananchi bila msaada, kama jambo hulifahamu vizuri tafuta ushauri kwa watumishi wenzako, suluhisho linaposhindwa kupatikana husisha ngazi za juu za uongozi hasa kama sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali haiwezi kutatua"Alisema Mahendeka.

Akatolea mfano wa uwepo wa baadhi ya taasisi ambazo pamoja na maelekezo na sheria kuwa wazi na kuwa na mamlaka kisheria, bado wamekuwa wakipeleka barua kuomba maelekezo au ridhaa ya kutatua au kufanya jambo fulani.

"Ni vyema mkafanya utafiti kabla ya kutoa ushauri na kumaliza kazi zenu ili ziwe timilifu badala ya kufanya kazi nusu nusu kwa kutegemea viongozi wenye fani zinazofanana kumalizia kazi hizo"Aliongeza

Akasema kuanzia sasa wataanza kufanya tathmini kuhusu utekelezaji wa majukumu yao na atakayebainika kuwa chimbuko la matatizo kwenye taasisi yake ataundiwa Kamati ya uchunguzi na hatua stahiki zitachukuliwa.

Akasema hatua zitakazochukuliwa zitahusisha taasisi za Serikali zinazozalisha Malalamiko mengi yasiyopatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu, taasisi zisizowasilisha taarifa au zinazochelewa kuwasilisha taarifa wanazoombwa.

Aidha akazielekeza Mamlaka za Rufaa kuchukua hatua za kinidhamu kwa taasisi za umma zilizogoma au kushindwa kutekeleza uamuzi wa Mamlaka hizo kwa Watumishi wa umma waliochukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2022 bila kuoneana aibu.

Mratibu wa idara ya utawala wa utumishi wa umma na malalamiko, ofisi ya Rais Ikulu,Hilda Lugembe, anabainisha bado kuna matundu mengi yanayoachwa na Watumishi hao katika masuala ya nidhamu na huduma kwa wateja.

Lugembe akasema lengo la mafunzo hayo yanayofanyika kwa awamu ya tatu baada ya yaliyokwisha fanyika Tanga na Iringa ni kufanikisha usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya nidhamu, Malalamiko, Rufaa na kero za Watumishi wa umma na wananchi ufanyike kwa haraka, ukamilifu na kupatiwa ufumbuzi Katika ngazi ya taasisi. 

Akataja malengo mengine kuwa ni kuwaondolea wananchi na Watumishi wa umma usumbufu wa kufuatilia majibu ya malalamiko na kero zao kwenye Mamlaka za juu kama vile kwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Katibu Mkuu kiongozi na viongozi wengine.

Aidha kuepuka gharama ambazo Serikali inaweza kulipia endapo umeshindwa kesi inayotokana na suala la hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi ya mtumishi wa Umma au mwenye madai dhidi ya Serikali.

Mengine ni Ili kuepusha wananchi wakiwemo watumishi wa Serikali kuchukia Serikali pale ambapo hawakuhudumiwa vizuri au malalamiko na kero zao hazikutatuliwa kwa wakati Kero za wananchi ama watumishi wa zinapofanyiwa kazi kwa haraka na wakati zinafanya waimaini zaidi Serikali yao na kushiriki ipasavyo katika shughuli za maendeleo.

Mratibu huyo pia akasema dhamira nyingine ni kuepusha viongozi wakuu wa nchi kutumia muda mwingine kusikiliza malalamiko na kero za wananchi na kuzitatua wakati Wana majukumu mengi ya kuliongoza Taifa kufikia mafanikio makubwa ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu mkuu ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Anyangwe Lupembe, alisema ofisi hiyo itaendelea kusimamia suala zima la Utawala bora katika kuzingatia sheria kanuni na taratibu mbalimbali kusaidia huduma kwa wananchi hivyo kutozingatia Sheria kunaisababishia hasara Serikali.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI