Header Ads Widget

MDAU AJITOLEA VITI VYA MIL.1.5 ZAHANATI YA ITEZI MBEYA

 


Na Josea Sinkala

Kampuni ya Kati Investment limited yenye makao yake makuu jijini Mbeya, imetoa na kukabidhi msaada wa viti vya kukalia wagonjwa katika Zahanati ya Itezi Uyole jijini Mbeya ili kuwasaidia wananchi hasa wanapokwenda kupata huduma katika Zahanati hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa kampuni hiyo Edeni Samweli Katininda, Afisa kutoka kwenye kampuni hiyo bwana Alfred Robert Mwakibete, amesema mkurugenzi na wafanyakazi walifikia hatua ya kukabidhi viti nane kwenye Zahanati hiyo ambapo kila kiti kina uwezo wa kukaliwa na watu watano.


Mwakibete amesema kwa muda mrefu, mkurugenzi wa kampuni hiyo Edeni Katininda na kampuni yake, amekuwa na utaratibu wa kutoa misaada katika maeneo mbalimbali ikiwemo kukarabati barabara, kufufua chanzo cha maji mto Lanzi na kupeleka maji hasa shuleni kutokana na baadhi ya maeneo hasa ya kata ya Itezi kuwa na upungufu wa huduma hiyo hivyo kuwaondoa hofu wanaodhani msaada huo umetolewa kwakuwa ni kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Kaimu mtendaji wa kata ya Itezi Tuyanje Patrick Tuyanje ameishukuru kampuni hiyo kwa kuona adha zinazowakumba wananchi waliokuwa wakienda kupata huduma katika Zahanati hiyo huku mwenyekiti wa ntaa wa Mwasote January Robert akishukuru na kuomba wadau wengine kujitokeza kusaidia uboreshaji mazingira ya Zahanati hiyo ikiwemo kujenga uzio na kuongeza majengo.


Doreen Lyimo ni mganga mfawidhi wa Zahanati ya Itezi, anasema wagonjwa walikuwa wakihangaika mahali pa kukaa kwani Zahanati hiyo ilikuwa na mabenchi machache hivyo wengine kulazimika kukaa kwenye nyasi adha ambayo sasa imepata suluhu.

Viti hivyo vina thamani ya shilingi million moja na nusu ambapo msaada wa mdau huyu wa maendeleo unapaswa kuigwa na wadau wengine kusaidia uimarishaji huduma kwenye sekta mbalimbali ili kuunga mkono juhudi za Serikali.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI