Header Ads Widget

GUMZO LA UCHAGUZI JIMBO LA IRINGA MJINI MCHUNGAJI MSIGWA AKITAJWA KUCHUKUA FOMU

  


Na Francis Godwin – Matukio Daima, Iringa

Joto la kisiasa katika jimbo la Iringa Mjini limezidi kupanda huku jina la aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi viwili kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa akiibuka  gumzo jipya baada ya kuhusishwa na nia ya kurejea katika kinyang’anyiro cha ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ingawa bado hajatangaza rasmi azma yake, maneno ya “No comment, daraja litajengwa tukifika mtoni” aliyoyatoa alipoulizwa na mwandishi wa Matukio Daima yamezua tafsiri nyingi miongoni mwa wakazi wa Iringa, wachambuzi wa siasa na wanachama wa CCM, huku wengi wakisema kauli hiyo ni dalili tosha kwamba Msigwa anapima upepo kabla ya kutangaza rasmi kurudi katika ulingo wa siasa za uchaguzi.


Jimbo la Iringa Mjini linatajwa kuwa ni moja ya majimbo ya kihistoria nchini, kutokana na mchanganyiko wa nguvu za kisiasa kati ya chama tawala na vyama vya upinzani kwa miongo kadhaa. 

Katika chaguzi zilizopita, jimbo hili limewahi kuwa ngome ya upinzani hususani kupitia NCCR MAGEUZI na CHADEMA ikiwa chini ya uongozi wa Mchungaji Msigwa aliyepata umaarufu mkubwa kutokana na ushujaa wake wa kulisemea bunge kwa sauti ya juu na msimamo thabiti.

Lakini baada ya msuguano wa muda mrefu ndani ya CHADEMA na hatimaye kujiondoa kwake katika chama hicho, Msigwa alijiunga na CCM na kuonekana akihudhuria mikutano na shughuli mbalimbali za chama hicho akiwa pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Taifa, Amos Makalla, jambo lililothibitisha kuwa hana mpango wa kustaafu siasa.

Katika mahojiano maalum ya Jukwaa la Siasa ya Matukio Daima TV, wakazi mbalimbali wa Iringa walieleza maoni yao kuhusu taswira ya siasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Shaban Alli, mkazi wa Kitwiru na kada wa CCM, alisema Iringa Mjini ni jimbo gumu kisiasa, linalohitaji mgombea mwenye ushawishi wa kweli.

 Alisema, “Hatutashangaa kama Mchungaji Msigwa atarudi tena katika ulingo wa ubunge kupitia CCM.


Kuwa hili  ni jimbo la kihistoria, linahitaji mtu anayejua mikikimikiki ya siasa na aliye tayari kusikiliza wananchi.”

Kwa upande wake, Zuwena Sanga wa Kihesa alisema, “Msigwa aliwahi kuwa mbunge wa wananchi alikuwa anapigania masuala ya wananchi bungeni hata kama alikuwa na mapungufu yake. 


kuwa kama atagombea tena, naamini ataungwa mkono na watu wengi hasa wale waliomkosa kwa muda.”

Asha Kalinga wa Nduli alieleza kuwa ushindani ndani ya CCM kwa sasa ni mkali zaidi kuliko wakati wowote ule.

 “Msambatavangu amefanya kazi, lakini baadhi ya watu hawaridhiki naye. Jimbo hili sasa linahitaji mtu mpya mwenye ushawishi wa kitaifa na uwezo wa kusikiliza wananchi wake. Msigwa ni miongoni mwa watu hao.”

FADHIL NGAJILO NA MBIO ZA AWALI

Hadi sasa, mwanasiasa pekee ndani ya CCM aliyethubutu kutangaza wazi nia ya kuwania ubunge jimbo la Iringa Mjini ni Fadhil Ngajilo, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa wa Iringa. 

Ngajilo, licha ya kuwa na nafasi ya uongozi ndani ya chama, bado hajapata uungwaji mkono mkubwa unaomlazimu kuwa na mkakati madhubuti wa kupenya katika kinyang’anyiro hicho chenye ushindani mkubwa.

Kitendo cha Ngajilo kugombea Iringa mjini na Mdogo wake Fredy Kugombea Kalenga inatajwa kama Uroho wa madaraka na kufanya ubunge wa kifamilia hivyo wanataka Fredy aachiwe kalenga na Fadhil amuunge mkono mdogo wake.

Baadhi ya wakazi wanamwona Ngajilo kama kiongozi mwenye maadili, lakini wanasema bado hajajipambanua vya kutosha kisiasa ukilinganisha na wanasiasa wenye historia kubwa kama Msigwa, Msambatavangu au hata mawakili na wanaharakati wanaotajwa kuwania nafasi hiyo pia hatua ya Ngajilo kutangaza kutaka ubunge tena jimbo hilo ikiwa ni awamu ya tatu sasa kutaka nafasi hiyo jimbo la Iringa mjini kuwa bado anayosafari na ipo siku itatimia ndoto yake.

KASORO NDOGO NDOGO ZA MBUNGE WA SASA

Mbunge anayemaliza muda wake, Jesca Msambatavangu, anatajwa kuwa na changamoto kadhaa ambazo baadhi ya wananchi wameziona kama kikwazo kwake kurejea bungeni.

 Ingawa amekuwa akiwakilisha chama vyema bungeni na kushiriki mijadala mbalimbali ya kitaifa, lakini wakazi wengi wanasema amekuwa akienda bungeni na mambo yake na  mara nyingi anatajwa kuwekeza muda mwingi katika mijadala ya kitaifa inayohusu masuala ya kijinsia, kama nguvu za kiume, badala ya kuzungumzia maendeleo ya jimbo lake.

“Kama kweli tunataka maendeleo ya Iringa Mjini, basi tunahitaji mbunge atakayekutana na wananchi wake mara kwa mara, kusikiliza kero zao na kuhakikisha kila hoja inayowagusa wananchi inawasilishwa bungeni hii tabia ya kujikita kwenye siasa za majukwaa ya kitaifa bila kujali hali ya watu wa jimbo, imeharibu wanasiasa wengi,” alisema mmoja wa wakazi waliohojiwa.

KINA WAKILI AMBWINDWILE NA NGUVU MPYA ZAJITOKEZA

Mbali na Msigwa, Msambatavangu na Ngajilo, kuna majina mengine kadhaa ambayo yanatajwa kuonyesha nia ya kuwania ubunge ndani ya CCM Watu kama Wakili Moses Ambwindwile, Islam Huwel, Nguvu Chengula na Ibrahim Ngwada ni baadhi ya wana CCM wanaotajwa kuandaa mikakati ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanasema kuwa majina haya ni mapya kwenye siasa za wakati huu  kwa sehemu kubwa ya wananchi wa Iringa Mjini, na kwamba wanahitaji kufanya kazi ya ziada kujijengea heshima, imani na ufuasi wa kweli kabla ya uchaguzi wa ndani wa chama.


Japo Nguvu Chengula na Ngwada walishagombea kura za maoni zilizompitisha Msambatavangu kwa Nguvu kushika nafasi ya pili na Ngwada kushika nafasi ya tatu ,huku Islam yeye ni mara ya kwanza kutajwa kutaka ubunge japo ni mjunbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa akiwakilisha wilaya ya Iringa mjini.

CCM YATAKIWA KUANDAA MGOMBEA MAKINI

Wakati wimbi la uchaguzi likizidi kupanda, baadhi ya wanachama wa CCM wanasema chama hakijaweka wazi mchakato wa maandalizi ya kupata mgombea wa ubunge katika jimbo la Iringa Mjini. 

Wengi wanatamani kuona mchakato wa ndani ukiendeshwa kwa haki, uwazi na ushindani halali ili kuhakikisha mgombea bora anayekubalika ndani na nje ya chama anapatikana.

“Hili si jimbo la mzaha hii ni Iringa Mjini Ukifanya kosa dogo tu, unaweza kupoteza jimbo lote tunahitaji mtu mwenye mvuto, hoja, maono na uwezo wa kweli wa kuunganisha watu wa tabaka zote,” alisema mmoja wa wajumbe wa CCM kata ya Makorongoni aliyeomba kutotajwa jina.

NO REFORM NO ELECTION: WAFUASI WA CHADEMA WAMLILIA MSIGWA

Wakati baadhi ya wanachama wa CCM wakimhitaji Msigwa kama mkombozi mpya, upande wa CHADEMA unaonekana kugawanyika. 



Wafuasi wa zamani wa Msigwa wanamsifu kuwa ndiye aliyekuwa sauti yao halisi bungeni hata hivyo, uamuzi wake wa kuhamia CCM bado unaumiza mioyo ya wanachama wa CHADEMA ambao wanaendelea kuamini katika msimamo wa “No Reform No Election”.

“Mimi ni CHADEMA damu najua chama kimesema hatutashiriki uchaguzi pasipo marekebisho ya mfumo lakini ikitokea kweli hatugombei, nitampigia kura Msigwa alikuwa anatuwakilisha vizuri bungeni Mbowe anaweza kumuita Yuda, lakini sisi tumeshajua ukweli Msigwa aliondoka kwa sababu ya msimamo wake, si usaliti,” alisema kijana mmoja wa Kihesa aliyekuwa mmoja wa wafuasi wa kampeni za CHADEMA mwaka 2020.

Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwa Mchungaji Peter Msigwa. Je, atavunja ukimya na kutangaza nia rasmi ya kurejea katika ulingo wa ubunge kupitia CCM? Je, chama hicho kitamkubali kuwa mgombea wake licha ya historia yake ya kuwa mpinzani mkali? Je, wananchi wa Iringa Mjini wako tayari kumpa tena ridhaa ya kuwakilishwa naye?

Kwa vyovyote vile, uchaguzi mkuu wa 2025 unakuja na sura mpya katika jimbo la Iringa Mjini, na kama kuna jina linalowasha moto wa gumzo mtaani, basi ni la Mchungaji Peter Msigwa.

Matukio Daima itaendelea kukuletea mfululizo wa makala maalum na mahojiano ya kina kuhusu uchaguzi mkuu ujao. Endelea kufuatilia Jukwaa la Siasa.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI